Serikali imeuagiza uongozi wa kiwanda cha kuchinja Punda Mkoani Shinyanga kusimamisha shughuli zake hadi hapo watakapotekeleza sheria na taratibu za uendeshaji wa kiwanda ikiwemo kuweka mifumo iliyoelekezwa ya kuteketekeza taka ngumu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Kangi Lugola ametoa agizo hilo wakati akikagua kiwanda hicho katika ziara yake ya siku moja Mkoani hapa tarehe 06/06/2018.
Mhe. Lugola ametoa siku 2 kwa kiwanda hicho, kuondoa mizoga na uchafu wote eneo la kiwanda pamoja na kushughulikia mizoga hiyo kwa namna bora inayotakiwa, hadi hapo Baraza la Taifa la Uhifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC) litakapofanya uhakiki na kuridhia kuendelea kwa shughuli kiwandani hapo.
Katika ziara hiyo imebainika kuwa, kiwanda kimekaidi maagizo ya Manispaa ya Shinyanga ya kuacha kuchoma mifupa na uchafu wa matumbo katika eneo la kiwanda licha ya kuagizwa kwa maandishi tangu mwezi Machi mwaka huu.
"Wamekuwa na mifumo duni isiyokidhi matakwa ya kimazingira, Serikali ya Rais Magufuli haimuogopi Mwekezaji anayevunja sheria na kukaidi maagizo ya Serikali" amesema Mhe. Lugola.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Lugola amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bw. Geoffrey Mwangulumbi kuhakikisha mitaro inayotoka kwenye machinjio ya Manispaa iliyopo katika eneo la Nguzo Nane, pamoja na Mitaro mingine yote ya aina hiyo, inazibuliwa na kusafishwa ndani ya wiki moja ili kuondoa harufu mbaya eneo hilo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa