Wadau wa Elimu Mkoani Shinyanga wameazimia kwa pamoja kuhakikisha tatizo la mimba kwa wanafunzi linakwisha kwa kuzitaka kila Halmashauri kuweka mkakati wa kutoa elimu ya kujitambua kwa watoto wa kike na kujenga shule angalau mbili.
Maazimio hayo yamefikiwa katika kikao cha kila mwaka cha wadau kilichojadili changamoto zinazoikabili sekta ya elimu Mkoani hapa, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela, suala la mimba za utotoni limechukua nafasi ya wadau kujadili kwa mapana na kufikia maazimio hayo ambapo wadau wamesisitiza kuwa, iwapo watoto wa kike watapata elimu ya kujitambua, itawasaidia kujiepusha na vishawishi vya kujiingiza kwenye matendo mabaya.
Maazimio mengine ni pamoja na kuendelea kuwapima wanafunzi wa kike ujauzito kila baada ya miezi mitatu, kuwataka watoto wa kike kutembea kwa makundi na pia kila shule kuwa na mwalimu wa kike angalau mmoja.
Pamoja na malengo hayo, wadau wameazimia kuhakikisha kila Halmashauri inaongeza vyumba vya madarasa na madawati ili kukabiliana ongezeko la wanafunzi kila mwaka wanaoandikishwa darasa la kwanza na wanaojiunga na kidato cha kwanza.
Aidha, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wamesisitizwa kuweka bajeti za kuboresha miundombinu ya shule zenye kidato cha tano na sita ili wanafunzi wanaofaulu kidato cha nne wapate nafasi katika shule hizo. Imesisitizwa pia kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri za Mji Kahama na Manispaa ya Shinyanga zijenge shule za kidato cha tano na sita ili kuongeza idadi ya wanafunzi waliofanya vizuri kidato cha nne.
Akifunga kikao hicho, Bw. Msovela amewataka kila mmoja afanye kazi kwa nafasi yake ili kuyatekeleza yote yaliyokubaliwa na kuondoa changamoto zinazoikabili Sekta ya elimu, aidha amepongeza Sekta binafsi kwa mchango wao wa kufanya Mkoa uwe katika nafasi nzuri ya ufaulu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa