Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka wahandisi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoa wa Shinyanga kusimamia ujenzi wa barabara kwa kiwango na kulingana na thamani halisi ya fedha.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko wakati wa ufunguzi wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa kilichofanyika leo tarehe 09/04/2019 Mhe. Telack amesema ni matumaini yake kuwa Wakala wa barabara Mjini na Vijijini TARURA watafanya kazi kwa ufanisi zaidi tofauti na hapo awali.
“Hakikisheni mnawasimamia wakandarasi wajenge barabara kulingana na thamani ya fedha na zinazodumu kwa muda mrefu”
Amesema Serikali ilianzisha Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini TARURA kwa lengo la kusaidia kupunguza changamoto zilizokuwepo awali ikiwemo usimamizi na utunzaji wa barabara.
Aidha, ameitaka TARURA kwa kushirikiana na Halmashauri pamoja na vyombo vya dola kuhakikisha magari yenye uzito mkubwa yanafuata sharia na hayapiti kwenye barabara zisizoruhusiwa.
“Barabara nyingi zilizo chini ya TARURA zinaharibika kutokana na magari yenye uzito mkubwa kupita kwenye barabara zilizo na uwezo wa kupitisha magari madogo”
Katika kikao hicho wajumbe wameipongeza TARURA kwa kufanya kazi nzuri Mkoani hapa hali iliyochangia barabara nyingi kuimarika tofauti na miaka ya nyuma.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa