Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita leo Septemba 20, 2025 ameongoza zoezi la usafi katika Soko la Kambarage, Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Usafishaji Duniani huku akibainisha kuwa soko hilo lipo mbioni kubomolewa ili kupisha ujenzi wa soko jipya la kisasa kupitia mradi wa TACTIC.

Akizungumza baada ya usafi huo, Mhe. Mhita amesema Serikali imeshapata fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya, na kwamba maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo yamekamilika, hivyo wananchi wanapaswa kujiandaa na mabadiliko hayo kwa mtazamo chanya.
“Mradi huu wa TACTIC utaliwezesha Soko la Kambarage kuwa la kisasa zaidi, lenye miundombinu bora ya biashara. Lakini pamoja na mabadiliko haya yanayokuja, tunapaswa kuendeleza tabia ya kufanya usafi wa mazingira wakati wote usafi ni afya, si jambo la kulazimishwa,” amesema Mhita.

Aidha, RC Mhita amewapongeza wananchi, wafanyabiashara, taasisi mbalimbali na wadau wote waliojitokeza kushiriki usafi huo, na kutoa rai kwa jamii kuendelea kushiriki katika utunzaji wa mazingira kwa maslahi ya afya ya jamii.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, amesisitiza kuwa zoezi la usafi halipaswi kuwa la siku moja au kwa ajili ya kumbukumbu, bali liwe sehemu ya maisha ya kila siku.

“Zoezi hili la leo lionesha mwitikio mzuri, lakini ni jukumu letu kuhakikisha usafi huu unaendelea kila wiki. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuifanya Shinyanga kuwa mkoa wa mfano katika usafi,” amesema CP Hamduni.
Kauli mbiu ya Siku ya Usafishaji Duniani kwa mwaka huu ni: “Tunza Mazingira kwa Kuzipa Taka Thamani” ikiwa na lengo la kuhamasisha uchakataji wa taka na matumizi mbadala kwa maendeleo endelevu.

OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa