Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amefungua soko la madini leo tarehe 03 Mei, 2019 katika Wilaya ya Shinyanga likiwa ni soko la pili baada ya soko jingine kufunguliwa Wilayani Kahama mwezi mmoja uliopita.
Akitoa hotuba ya ufunguzi wa soko hilo katika eneo la Ofisi ya CCM Mkoa ambapo wafanyabiashara tisa (9) wa Dhahabu na Almasi wamefungua masoko yao hapo, Mhe. Telack amesema tangu agizo la Mhe. Dkt. John Magufuli la kufungua masoko ya madini, tayari madini ya dhahabu yenye gramu 30,924.44 yameshauzwa katika soko la Kahama yakiwa na thamani ya sh. Bilioni 2.9.
Telack amewashukuru wafanyabiashara hao kwa kuitika wito wa Serikali na kufungua soko katika Mkoa wa Shinyanga.
Aidha, ametoa wito kwa wachimbaji wadogo, wauzaji na wanunuzi kutumia soko hilo la madini na waache kuuziana madini sehemu zisizo rasmi na atakayekamatwa anafanya hivyo madini yatataifishwa na wahusika watashtakiwa kwa mujibu wa sheria.
Kaimu Afisa Madini Mkazi Mhandisi Giliard Luyoka, akisoma taarifa ya madini Mkoa, amesema hadi sasa Mkoa una wafanyabiashara wakubwa 9 na wadogo 22 na kuwa licha ya Mkoa kuwa na utajiri wa madini yenye thamani ambapo wachimbaji wadogo wanazalisha wastani wa kilo 600 za dhahabu na karati 1300 za almasi kwa mwaka, hakukuwa na masoko rasmi ya uuzaji wa madini hivyo kupelekea utoroshwaji wa madini hatimaye Taifa kutonufaika na madini hayo.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Wachimba madini Mkoa wa Shinyanga Bw.Hamza Tandiko amesema kuwa, wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha madini yote yanayopatikana Mkoani Shinyanga yanawasaidia wananchi wa Mkoa huu kwa kuchangia pato la Taifa.
“Tuendelee kumuunga mkono Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, kufikia mwaka 2025 angalau sisi tuliopo kwenye sekta ya madini tuweze kuchangia angalau asilimia 10 ya pato la Taifa kwani Serikali imeonesha uzalendo kwa kufuta kodi hivyo deni limebaki kwetu” amesema Hamza.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa