Na. Paul Kasembo, KISHAPU.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamiringi Macha amewataka wafanyakazi na watumishi katika mgodi wa Williamson Diamonds Ltd (WDL) maarufu kama MWADUI kuwa wazalendo na waaminifu katika shughuli zao za uchimbaji na utunzaji wa madini mgodini hapo huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na kuwashirikisha ilI nao wanufaike.
RC Macha ameyasema haya tarehe 19 Agosti, 2024 alipofika mgodini hapo akiwa ameongozana na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde (MB) kwa lengo la kuangalia namna ambavyo mgodi unatekeleza majukumu yake, kusikiliza changamoto zao na kuona namna ya kuzishughulikia ili lengo la mgodi na Serikali liweze kufikiwa.
"Pamoja na kuwapongeza kwa kazi hii nzuri na yenye tija mnayoifanya, niwaombe watumishi wote katika mgodi huu kutanguliza uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yenu ili kazi hii iwe na tija zaidi na kufikiwa kwa lengo la kuongeza pato la Serikali na pia muendelee kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na muwashirikishe zaidi ili na wao wanufaike,“ amesema RC Macha.
Akitoa taarifa ya uzalishaji, Meneja Mgodi wa Almasi wa Mwadui ndg. Ayoub Mwenda amesema kuwa uzalishaji kwa sasa umeongezeka lakini wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo moja kubwa ya kushuka kwa soko la Almasi duniani.
Ayoub amesema, kushuka kwa soko kumesababisha kupata mauzo hafifu ya Almasi licha ya kuwa na uzalishaji mkubwa jambo linalopelekea kupunguza matumizi ambayo siyo ya lazima ikiwa ni pamoja na kupunguza watoa huduma ndani ya mgodi.
Kwa upande wake Mhe. Mavunde amesema kuwa, changamoto ya kushuka kwa soko la madini ya Almasi ni ya dunia nzima na siyo Mwadui pekee, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na Mgodi wa Almasi Mwadui kutatua changamoto hiyo ili kurudisha heshima na hadhi ya madini ya Almasi.
"Changamoto hii ya kushuka kwa soko la madini ya Almasi zipo sababu kuu 4,moja ikiwa ni kuwapo kwa uzalishaji wa madini ya Almasi za Maabara ambazo bei zake ni za chini," amesema Mavunde.
Aidha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mheshimiwa Masache Kasaka amewakumbusha viongozi wa Mgodi wa WDL kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na Kamati kwa wakati kama yalivyoelekezwa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa