Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimetakiwa kushirikiana katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto zinazosababisha uharibifu wa barabara na mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Bodi ya barabara kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi yake Mkoani hapa.
Mhe. Telack amesema, TANROADS pamoja na Halmashauri zote waunganishe nguvu katika kutoa elimu kwa wananchi japokuwa wakati mwingine ni wananchi wenyewe kutojali hali inayosababisha barabara kuharibika mapema.
"Kumekuwa na changamoto nyingi katika Sekta ya barabara katika Mkoa wetu zikiwemo wananchi kutokujali au kutoelimishwa vya kutosha juu ya utunzaji wa Barabara kwa kulima, kujenga, kufanya biashara ndogo ndogo na hata kuegesha magari kwenye hifadhi ya barabara, hii huchangia barabara hizo kuharibika mapema na wakati mwingine kuzifanya zisipitike kwa urahisi hasa sehemu za miji yetu na Makao Makuu ya Wilaya".
Aidha, Mhe. Telack amewataka Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani Shinyanga kuwapa maelekezo Wakuu wa shule ili wawaelimishe watoto namna ya kuvuka barabara pamoja na athari za kutokuwa makini katika uvukaji wa barabara ili kupunguza ajali za watoto kugongwa na magari mara kwa mara.
Baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo wakichangia katika kikao hicho pia wameungana na Mhe. Mkuu wa Mkoa na kutaka sheria ndogo zitumike kuwabana wananchi wanaokiuka matumizi sahihi ya barabara pamoja na kuongeza juhudi katika kutoa elimu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa