Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)imetoa elimu kwa waandishi wa Habari wa Mkoa wa Shinyanga kuhusu huduma ya kuhama mtandao pasipo kubadili namba ya simu.
Elimu hiyo imetolewa mapema leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kuwafikia wananchi na wadau wa mawasiliano kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Mhandisi Mwesigwa Felician ambaye ni Mhandisi Mwandamizi wa huduma za mawasiliano wa TCRA amesema kuwa, huduma hiyo ni ya hiyari ambayo inamuwezesha mtumiaji wa simu kuhama kutoka mtandao anaoutumia na kuamua kutumia mtandao mwingine kwa namba ileile moja bila usumbufu wowote kwa ndugu, jamaa na marafiki.
Bw. Mwesigwa amesema faida kubwa ya huduma hii ni pamoja na mteja kuchagua mtoa huduma ambaye anaona anatoa huduma bora zaidi kwa wateja na anayekidhi matarajio ya mteja.
Aidha, huduma hii inachangia kuongeza ushindani kati ya watoa huduma za mawasiliano hivyo kuwa kichocheo cha utoaji huduma bora na zenye gharama nafuu kwani wateja watahama kufuata huduma bora.
Naibu Mkurugenzi wa masuala ya watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano wa TCRA Bw. Thadayo Ringo amesema kuwa huduma hiyo ni bure na mwananchi anaweza kuhama wakati wowote anaohitaji kwa kutembelea vituo vya mauzo au mawakala akiwa na kitambulisho chenye picha yake pamoja na simu ya kiganjani yenye namba anayotaka kuhamia.
Bw. Ringo amesisitiza wananchi kuwa makini kwenye matumizi ya simu ikiwemo matumizi ya miamala ya fedha kwa kuhakikisha makosa ya uzembe hayajitokezi hivyo kuepuka usumbufu wa kutorudishiwa fedha zao.
Amewataka wananchi kutoa taarifa au malalamiko wakati wowote wanapojikuta wanapata usumbufu katika matumizi ya simu au huduma za mawasiliano.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa