Na. Paul Kasembo, SHY MC,
WAZIRI wa Uchukuzi nchini Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na wataalamu tayari wameanza kufanyia kazi maelekezo ya Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye aliagiza kufungwa taa kwenye uwanja wa ndege wa Ibadakuli mkoani Shinyanga na mpaka sasa tayari wameagiza vifaa ili kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa ipasavyo ili uwanja huu ufanye kazi masaa 24 huku wakisubiria jengo la abiria kukamilika ambalo kwa sasa limefikia asilimia 50.
Prof. Mbarawa ameyasema haya Februari 20, 2025 wakati akikagua ujenzi wa jengo la abiria lililopo uwanja wa ndege wa Shinyanga ambapo ameongeza kuwa huu ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alitoa maelekezo mahususi kwamba uwanja huu wa ndege wa Ibadakuli pamoja na viwanja vingine vikarabatiwe na kuanza kutumika tena kama ilvyokuwa awali, hivyo anaamini kuwa uwanja huu utakamilika na kuanza kutumika kwa muda uliopangwa.
“Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na wataalam mbalimbali tayari tumeanza kufanyia kazi maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambaye aliagiza uwanja huu uwekewe taa na uanze kufanya kazi kwa masaa 24, hivyo mpaka sasa tayari tumeagiza vifaa ambayo vitatumika ili kuhakikisha uwanja huu unakamilika na kuanza kufanya kazi tena kama ilivyokuwa awali,” amesema Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amemshukuru sana Waziri wa Uchukuzi kwa kutembelea ili kufahamu maendeleo ya ukarabati mkubwa wa uwanja huu lakini pia ameshukuru kwa jitihada zilizofanyika ili kuboresha uwanja licha ya kwamba changamoto mbalimbali zilizojitokeza na kupelekea kucheleweshwa kwa ukarabati.
Kukamilika kwa uwanja wa ndege wa Ibadakuli mkoani Shinyanga kutafungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Shinyanga na maeneo ya jirani ikiwemo Simiyu, Geita na viunga vyake na hivyo kurahisisha usafiri wa watu na mizigo ambapo awali walikuwa wanasafiri Kilometa zaidi ya 164 kwenda Mwanza kupanda ndege.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa