Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ametoa wito kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha inatatua changamoto za wafanyabiashara kwa njia ya mazungumzo badala ya kufunga biashara, hasa pale ambapo matatizo hayo yanaweza kutatuliwa bila kuvunja sheria.
Mhe. Mhita aliyasema hayo leo, Septemba 10, 2025, wakati wa uzinduzi rasmi wa Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara kwa Mkoa wa Shinyanga, uliofanyika katika viwanja vya Ofisi za TRA.
Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji, hivyo ni muhimu kwa taasisi za mapato kutekeleza wajibu wake kwa kutoa elimu na kushirikiana na wafanyabiashara badala ya kutumia nguvu ya kufunga.
“Wafanyabiashara ni washirika wetu katika maendeleo. Kama kuna dosari, tusitafute njia rahisi ya kufunga biashara bali tuwasaidie kurekebisha na kuelewa wajibu wao. Changamoto zinazotatulika zisigeuzwe kuwa adhabu,” alisema Mhe. Mhita.
Awali, Meneja wa TRA Mkoa wa Shinyanga, Bw. Emmanuel Maro, alieleza kuwa kuanzishwa kwa dawati hilo ni hatua muhimu ya kuimarisha mahusiano ya karibu na wafanyabiashara kwa kuwapa elimu ya kodi, kuwalea katika biashara zao na kuwasaidia kufikia ndoto zao bila vikwazo visivyokuwa vya lazima.
“Dawati hili litatumika kama daraja la mawasiliano kati ya TRA na wafanyabiashara, kuwasaidia kwa njia ya kitaalamu ili waongeze tija na kuchangia kikamilifu pato la taifa,” alisema Maro.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa