Kampuni ya simu Tanzania imezindua rasmi huduma za 3G/4G katika Mkoa wa Shinyanga katika hafla fupi iliyofanyika leo kwenye viwanja vya Ofisi ya TTCL Mkoa ikiwa ni kutekeleza mpango mkakati wake wa Biashara wa miaka mitatu 2016 -2018 unaolenga kuboresha na kuleta huduma mpya katika soko na kuongeza tija na uwajibikaji.
Akizindua huduma hiyo, Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amesema kuwa uzinduzi wa huduma hii ni wa kipekee kwa TTCL na Sekta nzima ya mawasiliano Mkoani na Tanzania kwa ujumla.
Amewaomba wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kutumia mtandao wa simu wa TTCL ambayo ni mali ya Watanzania kwa asilimia 100.
"Wito wangu kwa Wananchi na Wakazi wa Mkoa wa Shinyanga, Turudi Nyumbani, tutangulize uzalendo kwanza kwa kutumia huduma za TTCL ambayo ni Kampuni yetu ya kizalendo na mali ya Watanzania kwa 100%"
Ameipongeza pia kampuni ya TTCL kwa kusimamia na kuendesha miradi mikubwa ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na Kituo cha Kimataifa cha kutunzia kumbukumbu.
Aidha, Mhe. Telack ameitaka kampuni ya TTCL kubuni mbinu za kujitangaza na kuvutia wateja, ishindane sokoni na iongoze kwa kuwajali wateja na kutoa huduma bora za uhakika zenye gharama nafuu ambazo wananchi wa kawaida watazimudu ili wananchi wapate sababu za msingi za kurudi kutumia mtandao wa TTCL.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Bw. Waziri Waziri Kindamba amesema kuwa uzinduzi huu unaongeza idadi ya Mikoa iliyofikiwa na huduma hii kuwa 16 katika Tanzania Bara ambapo ameongeza kuwa, huduma hii imeshafika pia na Tanzania Visiwani yaani Unguja na Pemba.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa