Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita , ametoa wito kwa viongozi wa dini mkoani humo na Nchini kwa ujumla kuendelea kusali na kuliombea Taifa, wananchi na viongozi, ili kudumisha amani, mshikamano na upendo hususan katika kipindi hiki tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mhe. Mhita ametoa wito huo leo, Oktoba 1, 2025, wakati wa Ibada ya Ufunguzi wa Mkutano wa 22 wa Ushirikiano wa Kimisioni ya Kilutheri (22nd LMC Roundtable Meeting) uliofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania – Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria (KKKT-DKMZV), Shinyanga, ambapo mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, Serikali na washirika wa kimataifa.
“Nitoe wito kwa viongozi wa dini kuendelea kusali kwa ajili ya taifa letu, viongozi na wananchi ili tuendelee kuwa na amani, umoja, mshikamano na uchaguzi wetu mkuu ufanyike kwa utulivu na upendo,” alisema RC Mhita.
Aidha, Mhita amewahakikishia washiriki wote wa mkutano huo kuwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu na kuhakikisha mazingira ya mkutano ni salama na tulivu wakati wote. Alisisitiza umuhimu wa kutumia mkutano huo kama fursa ya kubadilishana uzoefu, maarifa na maombi kwa ajili ya kulijenga Taifa kiroho na kijamii.
Hata hivyo RC Mhita ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwenye Uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 29,2025 ambapo amewahakikishia kwamba siku hiyo kutakuwa na utulivu wa kutosha ikiwa ni pamoja na Amani kwa wale wote watakaojitokeza kupiga Kura ya kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanisa la KKKT nchini, Dkt. Alex Malasusa, amesema mkutano huu ni jukwaa muhimu la kuendeleza huduma za kiinjili, kijamii na kimaendeleo huku akihimiza waumini kushikamana katika imani, haki na upendo kama njia ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Mkutano wa 22 wa LMC umebeba kaulimbiu ya kuimarisha ushirikiano kati ya KKKT na mashirika ya kimisheni Duniani kwa ajili ya huduma endelevu na maendeleo ya jamii na kanisa.
OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa