Na. Paul Kasembo, KAHAMA MC.
IKIWA ni siku ya sita (6) ya zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kwa Mkoa wa Shinyanga, kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama wananchi wamepokea zoezi kwa hamasa kubwa zaidi jambo ambalo limepelekea kwa baadhi ya maeneo ikiwemo kituo cha Shule ya Msingi Bukondamoyo kuongezwa BVR na kufikia nne (4) sasa huku Mratibu wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura Mkoa wa Shinyanga ndg. Bakari Kasinyo akitoa wito kwa wananchi kutumia vizuri muda uliobakia ili kupata huduma katika vituo mbalimbali vilivyopo katika maeneo yao.
Kwa mujibu wa Elikana Shija ambaye ni Afisa Uchaguzi Halmashauri ya Manispaa ya Kahama amesema kuwa mwitikio huu ni matokeo ya juhudi na kazi kubwa iliyofanywa na ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama kwa kutoa matangazo na hamasa ambapo walitumia njia mbalimbali ikiwemo magari ya matangazo, redio za kijamii, mabango, mikutano nk.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama ndg. Masoud Kibetu amesema kuwa, kila siku asubuhi yeye mwenyewe kabla ya kuingia ofisini huanzia kwenye vituo vya Uboreshaji Daftari la Mpiga Kura ambapo hukagua ili kuona kama kuna changamoto yoyote na kuzitatua na kisha huendelea na majukumu mengine lengo ni kuhakikisha kila kitu kinatekelezeka vema.
Mkoa wa Shinyanga unatekeleza zoezi hili ulioanza tarehe 21 Agosti, 2024 na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 27 Agosti, 2024 ambapo kila siku vituo hufunguliwa saa 2:00 asubuhi na hufungwa saa ifikapo saa 12:00 jioni.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa