Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amezindua wiki ya maadhimisho ya upandaji miti kwa kupanda miti zaidi ya 1000 katika kijiji cha Mwatuju, Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa maadhimisho hayo uliyofanyika leo, Mhe. Telack amewataka wananchi kuacha kusubiri mkono wa sheria uwaangukie isipokuwa kila mmoja atekeleze majukumu yake katika kupanda miti na kuitunza ili kuepuka na tatizo la jangwa linalonyemelea Mikoa ya kanda ya Magharibi kwa kasi
Telack amewataka wadau wa mazingira wajikite katika Mkoa wa Shinyanga kwani bado kazi ni kubwa kuhakikisha Mkoa unatoka katika hali ya Jangwa.
“Shinyanga siyo Jangwa, Jangwa tumelitafuta wenyewe. Kuirudisha Shinyanga katika hali yake na kuwa na misitu inawezekana” amesema Mhe. Telack.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Aggrey Mwanri ambaye ameambatana na Mhe. Telack katika uzinduzi huo, amesema wananchi wakipata elimu na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa za kuhifadhi mazingira, miti inayopandwa itaota na kuwasaidia katika ustawi wao ikiwemo kupata mvua za kutosha.
Maadhimisho haya ambayo yanafanyika kila mwaka tarehe 3 – 5 Aprili, mwaka huu yanafanyika kitaifa Mkoani Shinyanga, katika Wilaya ya Kishapu.
Kupitia maadhimisho haya, Mkoa utapanda zaidi ya miti 200,000 katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa.
Kilele cha maadhimisho ya upandaji miti kitaifa ni tarehe 5 Aprili, 2018 ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamis Kigwangala.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa