Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameushauri uongozi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Shinyanga (VETA) ukiongozwa na Mwl. Abraham Mbughuni kuanzisha na kusajili Kitengo Maalum cha Kuimarisha Uwezo wa Kujitegemea (Self Reliance Unity) kitakachokuwa na wajibu wa kubuni na kutekeleza kazi mbalimbali kwa kutumia rasilimali walizonazo ikiwemo wanachuo, mitambo na wakufunzi lengo likiwa ni kuzalisha kipato cha chuo huku akisema kuwa Serikali itafanya kazi pamoja nao ikiwa ni pamoja na kuwapatia zabuni za kujenga miradi ya Serikali.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 22 Novemba, 2024 wakati wa Mahafali ya 43 hafla iliyofanyika katika Viwanja vya VETA Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, wazazi/walezi, watumishi wa VETA, wananchi na wanachuo wenyewe ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wahitimu kwenda kuchangamkia fursa za mikopo ya Serikali isiyokuwa na riba pamoja na kuchapa kazi kwa bidii zaidi.
"Pamoja na pongezi kwako Mkuu wa Chuo na watumishi wote, lakini niwatake sasa kuanzisha Kitengo Maalum cha Kuimarisha Uwezo wa Kujitegemea (Self Reliance Unity) ambacho kitasajiliwa na kutambulika chenye lengo la kuzalisha, kukiwezesha chuo hiki kufanya kazi za nje, kuongeza pato na kukifanya chuo kujitegemea na kuchechemua uchumi wenu kupitia Fani mnazofundisha ikiwemo utengenezaji wa barabara na Serikali itafanya kazi pamoja nanyi na kuwashika mkono kwa kuwa mna kila kitu hapa ikiwemo mitambo mizito ya kutekelezea kandarasi za aina yoyote," amesema RC Macha.
Akitoa taarifa ya Chuo, Mwl Abraham amesema kuwa VETA Shinyanga ina jumla ya Ekari 19 zenye Hati Miliki, mazingira rafiki, tulivu na yenye kuvutia kwa kufundishia, kujifunzia, kupumzikia, mabweni, vyumba vya madarasa, karakana, maeneo ya kufundishia pamoja na kutoa taaluma kwa fani ya uendeshaji mitambo mizito, magari, uchomeleaji na uunganishaji vyuma huku akiwakaribisha wananchi kuleta kazi zote zinazohusu fani hizo kwani VETA inapokea na kutekeleza kwa ufanisi na weledi mkubwa zaidi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa