Na. Paul Kasembo, NGOFILA - KISHAPU
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewataka vijana wasomi mkoani hapa kuiga mfano wa vijana wa Jenga Kesho yako Bora (BBT) waliopo Kata ya Ngofila wilayani Kishapu ambao waliamua kujitolea na kuitumia elimu na maarifa yao yote katika kusaidia wakulima na kuamua kulima mashamba yao ya mfano kwa wakulima ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa taaluma waliyoipata Chuoni na kwenye mafunzo maalum ya BBT.
Hayo ameyasema leo Februari 18, 2025 wakati wa ziara ya kukagua na kuhamasisha kilimo cha zao la pamba katika Kata ya Ngofila wilayani Kishapu ambapo ametembelea Kijiji cha Mwamanota, Idushi na Ngofila ambapo huko amekutana na vijana hao wenye ari, nguvu na moyo wa dhati wa kutumia elimu na muda wao wote katika mashamba ya wakulima na ya kwao ikiwa ni sehemu ya kujipatia kipato, kujiajiri na hivyo kuwa sehemu ya mfano na chachu kwa vijana wengine.
"Niwashauri vijana na wasomi wetu mkoani Shinyanga, njooni muige na kujifunza namna bora ya kujiajiri na kutumia vema nguvu, elimu na maarifa mliyonayo huku Kata ya Ngofila wilayani Kishapu ambapo kuna vijana wenzenu kutoka kundi la Jenga Kesho iliyo Bora ambao wameamua kujitolea na kutumia elimu, maarifa na muda wao kuwasaidia wakulima katika kilimo cha pamba na wao pia kulima mashamba ya mfano ikiwa sehemu ya kujiajiri na kuongeza pato binafsi," amesema RC Macha.
Aidha, RC Macha amesema kuwa kwa sasa atakuwa anapatikana zaidi vijijini ambako ndiyo walipo wakulima na kwamba atatumia muda mwingi zaidi kuhamasisha na kuwatia moyo wakulima wote ili kuhakikisha heshima na hadhi ya pamba mkoani Shinyanga inarejea kama ilivyokuwa hapo awali, kwani pamba (dhahabu nyeupe) ni sehemu ya utambulisho wa Mkoa wa Shinyanga.
Akitolea mfano wa shamba la Raphael Zengi mkulima wa Kijiji cha Ngofila ambaye msimu wa 2023/2024 alipata kilo 4605 kwa hekari 4 ambapo ni wastani wa kilo 1150 kwa hekari moja, RC Macha amesema huo ndiyo mlengo na nia ya Serikali ya kuhakikisha kila mkulima anapata kuanzia kilo 1000 au zaidi kwa hekari moja.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa