Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewashauri viongozi wa dini Mkoani Shinyanga kufika vijijini kutoa masomo ya kiimani kwa wananachi ili wapate hofu ya Mungu na kupunguza vitendo vya uhalifu ikiwemo mauaji.
Mhe. Telack ameyasema hayo katika mkutano na wananchi wa kata ya Bunambiyu Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga akiwa kwenye ziara yake ya kukagua shughuli za kilimo na elimu anayoendelea nayo Mkoani hapa.
Telack amesema kuwa iwapo wananchi watakuwa na hofu ya Mungu kutokana na Imani ya dini hawawezi kuuana, kwani kumekuwa na matukio mengi ya wananchi kuuana katika kata hiyo hali inayosababisha kuharibu sifa ya Bunambiyu, Wilaya ya Kishapu na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla pamoja na kuwa ni kata yenye ardhi nzuri.
Amewataka kuacha kuchukua sheria mkononi kwa sababu ya ugomvi wa ng’ombe au wizi badala yake watoe taarifa za uhalifu Polisi, kwa Mkuu wa Wilaya au yeye mwenyewe itakapobidi.
Amesema vyombo vinavyoshghulika na sheria vipo, hivyo hataki kusikia tena mauaji katika kata hiyo kuanzia sasa kwani wahalifu wakikamatwa watapata hukumu inayostahili kutokana na makosa wanayofanya.
Amesema pia mwananchi yeyote atakayekamatwa na kosa la kuchukua sheria mkononi atakamatwa na kupewa adhabu inayostahili kwa sababu ndiyo utaratibu wa Serikali, hivyo wenye tabia hiyo waache mara moja.
Wakati huo huo Mhe. Telack amewataka viongozi wa vijiji kuwa na utaratibu wa kuwa na mikutano ya vijiji ili kupunguza majungu na hisia mbaya kwa wananchi.
Amesema kuwa uwazi kwenye kila jambo ikiwemo kutoa taarifa za miradi inayotekelezwa kutokana na michango ya wananchi.
“Tunataka uwazi kwa kila kitu, wananchi waambiwe fedha zao zimefanya nini, wakisema hawapati taarifa ya mapato na matumizi tunawakamata viongozi ili kujiridhisha fedha iliyochangwa imefanya kazi gani, ndiyo utaratibu”
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa