Watumishi wa Afya wametakiwa kutoa huduma kwa wananchi kwa moyo kwa kuzingatia maadili na kanuni za taaluma walizonazo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack ametoa wito huo hivi karibuni katika kikao cha kutambulisha mradi mpya wa kudhibiti maambukizi ya Kifua Kikuu unaofadhiliwa na "Global fund".
Mhe. Telack amesema kuwa, watendaji wa afya hasa Madaktari wasiridhike na maelezo ya wagonjwa tu ni wajibu wao kufanya uchunguzi zaidi ili kuibua magonjwa yaliyojificha na kuyatafutia tiba.
"Watendaji wa afya watoe huduma kulingana na taaluma zao, wazitendee haki na rasilimali zilizopo zitumike kwa ajili ya wagonjwa" amesema Telack.
Akizungumzia mradi huo, Mkuu wa Mkoa amewashukuru waratibu na kusema kuwa, tatizo la Kifua kikuu bado ni kubwa hapa nchini kwani Tanzania ni mojawapo ya nchi 30 Duniani zenye kiwango kikubwa cha ugonjwa huu kwa kuwa na wananchi 287 kati ya 100,000 wanaougua kila mwaka.
Naye Meneja mradi wa "Global fund" Bw. John Lyimo amesema mradi huo unaoendeshwa na mradi wa "Management and Development for Health" (MDH) ni wa mwaka mmoja ambapo Wagonjwa wa Kifua Kikuu watafuatwa majumbani kwa ajili ya kupewa elimu, ushauri na uchunguzi.
Aidha, mashine 189 za uchunguzi wa ugonjwa wa Kifua Kikuu zimeshawasili nchini na tayari Mkoa wa Shinyanga unazo mashine 6.
Bw. Lyimo amesema pia kuwa, mradi utafanya kazi katika maeneo makuu manne ambayo ni Migodini, Shule za bweni, Waganga wa jadi na kwenye mikusanyiko ya watu.
Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Rashid Mfaume amesema pia kuwa, ugonjwa wa Kifua Kikuu umeshamiri sana katika Migodi na shule za bweni.
Mradi huu utasaidia wagonjwa na wananchi kwa ujumla kuwapunguzia gharama za matibabu kwani mgonjwa mmoja kupona inagharimu jumla ya shilingi za Kitanzania milioni 8 hadi 9 katika utaratibu wa kawaida wa matibabu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa