Na. Paul Kasembo, SHY DC.
Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ndg. Gerson Msigwa ametoa wito kwa wakulima wa zao la pamba mkoani Shinyanga kuachana na kilimo cha mazoea na kuanza kutumia mbinu za kitaalamu ili kuongeza uzalishaji na wenye tija.
Akizungumza Mei 3, 2025 katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika katika Kijiji cha Sayu, Kata ya Pandagichiza, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Msigwa alisema Serikali imedhamiria kumsaidia mkulima kwa vitendo kupitia uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kutoa zaidi ya Tzs. Mil 17 kwa ajili ya kukuza kilimo cha pamba katika Mkoa huu.
“Natoa wito kwa wakulima wote wa zao la pamba hapa mkoani Shinyanga kuanza kutumia njia za kisasa na kitaalamu ukizingatia Serikali imalenga kumtoa mkulima kutoka kwenye kilimo cha mazoea kwenda kwenye kilimo chenye tija, na ndiyo maana tumewekeza Tzs. Bilioni 17 kwa ajili ya kukuza na kuboresha kilimo, hususan zao la pamba,” alisema Msigwa.
Aliongeza kuwa Serikali imepeleka vifaa vya kupima udongo vitakavyomuwezesha mkulima kutambua aina ya udongo na mazao yanayofaa kulimwa, pamoja na vifaa vya kisasa vya umwagiliaji. Vilevile, Maafisa Ugani wameajiriwa, kupatiwa mafunzo na vifaa vya kazi ili waweze kuwahudumia wakulima kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Msigwa, katika msimu uliopita, uzalishaji wa pamba ulikuwa takribani tani Mil 22, ambapo kwa wastani, kila hekari ilizalisha kilo 300 pekee – kiwango ambacho ni kidogo. Kupitia msukumo, usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringa Macha na mbinu bora za kilimo, na sasa Serikali imalenga kuona uzalishaji huo ukiongezeka hatua itakayoongeza thamani ya zao hilo na kuwapa wakulima motisha zaidi.
Huu ni muendelezo wa ziara za Msigwa kama Msemaji Mkuu wa Serikali katika Mikoa akielezea umma juu ya kazi zinazofanywa na Serikali katika Mkoa husika na Taifa kwa ujumla kupitia Sekta mbalimbali
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa