Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani Shinyanga kusimamiana wenyewe katika utendaji kazi na kuhakikisha hakuna hoja zisizokuwa za lazima wakati wa ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Mhe. Telack amesema hayo leo tarehe 25/06/2019 katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Kahama kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.
"Nawapongeza watumishi wa Halmashauri ya Mji Kahama kwa kuhakikisha hoja zote za hovyo hovyo zimeondoka tofauti na miaka mitatu iliyopita, ambapo kulikuwa na hoja nyingi zinazojibika kwa wakati na zisizokuwa na mashiko, hivi sasa zimeondoka" amesema Telack.
Ameisisitiza Menejimenti ya Halmashauri ya Mji Kahama kuendelea kuondoa hoja zisizo za msingi, huku akitoa pongezi kwa kupata hati safi kwa miaka sita mfululizo.
Aidha ametoa wito kwa Halmashauri zote wa kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali Mkoani hapa kwani imekuwa msaada mkubwa kwa Serikali ya Mkoa katika kudhibiti na kuzuia matumizi mabaya ya fedha za Umma.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amewataka watumishi wote wa Umma kufuata Sheria,kanuni na taratibu na kila mtumishi asimame kwenye nafasi yake ili kuzuia hoja nyingi zisizokuwa na sababu.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa