Na. Paul Kasembo, Shy RC.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewasisitiza Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari mkoani Shinyanga kufanya kazi kwa bidii na weledi wawapo mashuleni ili kuboresha na kuinua ufaulu kwa wanafunzi na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri za ufaulu kitaifa kwani kwa muda mrefu mkoa hauna matokeo mazuri.
RC Macha ameyasema haya leo Aprili 4, 2025 wakati akifungua Kikao Kazi na Wadau wa Elimu mkoani Shinyanga kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Shinyanga, kikao ambacho kimehusisha na kuhudhuriwa na Wadau wakiwemo Walimu, Wakufunzi wa Vyuo na Viongozi wa Serikali kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Kishapu na Shinyanga DC.
“Ninawasisitiza sana Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari mkoani hapa, baada ya kikao hiki muende mkafanye kazi kwa bidii na weledi muwapo mashuleni ili kuboresha na kuinua ufaulu kwa wanafunzi shuleni na hivyo kuufanya mkoa uwe kwenye nafasi nzuri za ufaulu kitaifa kwani ni muda mrefu sasa hatuna matokeo mazuri” amesema RC Macha.
Awali akimkaribisha RC Macha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Ndg. David Lyamongi alieleza kuwa Kikao Kazi hiki kimelenga kufanya tathmini ya elimu ya mwaka mmoja na miaka kadhaa iliyopita ili kuona ni kwa namna gani mkoa unaweza kupiga hatua na kusonga mbele kwenye sekta ya elimu.
Kwa upande Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Ndg. Samson Hango akiwasilisha Taarifa ya Elimu ya mkoa ya takribani miaka 9 kuanzia mwaka 2015-2023 amesema mkoa umekuwa hauna matokeo mazuri hususani kwa Shule za Msingi na kwa baadhi ya masomo katika Shule za Sekondari, hivyo amewataka Walimu wakajitathmini na kuona namna bora ya kuboresha na kuinua ufaulu wa wanafunzi kuanzia sasa.
Aidha wadau wa elimu mkoani Shinyanga Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari za Serikali pamoja za kibinafsi, Maafisa Elimu Kata pamoja na viongozi wengine kwa pamoja, wameshukuru kwa uwepo wa kikao kazi hiki kwani kimewasaidia kufahamu walikotoka na wanakoelekea kwenye sekta ya elimu huku wakiahidi kwenda kuyafanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na RC Macha.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa