Serikali Mkoani Shinyanga imeweka mikakati wa kuwasaidia wanafunzi wa kike waliofikia umri wa kupata hedhi kwa kuwawekea sehemu maalumu na salama za kujihifadhi wakiwa shuleni.
Mikakati hiyo imewekwa hapo jana katika Mkutano wa uhamasishaji wa masuala ya Afya ya uzazi kwa vijana ulioandaliwa na shirika la "amref health africa" chini ya wa mradi wa "DREAMS" wenye lengo la kuboresha afya ya uzazi kwa vijana.
Washiriki wa Mkutano huo uliowahusisha Viongozi, watendaji wa Serikali na baadhi ya wadau wa masuala ya Afya ya uzazi wamesema wanafunzi wengi wa kike wanashindwa kuhudhuria masomo wanapokuwa kwenye hedhi hivyo kupelekea utoro au kuacha shule kutokana na kutokuwa na mazingira rafiki ya kujihifadhi.
Washiriki hao wameiomba Serikali kuliangalia suala hilo kwani ni moja ya changamoto inayowakwamisha baadhi ya wasichana kutimiza ndoto zao kwa kushindwa kumaliza masomo na kuishukuru "amref" kwa kwenda hadi vijijini kutoa Elimu ya Afya ya uzazi kwa vijana.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amesema suala la muhimu hivi sasa ni kuziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa zote Mkoani hapa, kutumia miundombinu iliyopo kutenga mazingira hayo muhimu kwa wasichana wakati maandalizi ya kuweka maeneo hayo vizuri zaidi yakiendelea.
Mikakati mingine iliyowekwa katika Mkutano huo ni pamoja na kuweka suala la kutokomeza mimba za utotoni kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya ngazi zote kuanzia Mkoani.
Hali kadhalika, kuwakutanisha wadau wote wanaotekeleza Afua mbalimbali zinazofanana kuhusu Afya ya uzazi kwa vijana, ili waweze kuona namna ya kuunganisha nguvu katika kumlinda mtoto wa kike na vijana kwa ujumla.
Awali akisoma hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack, Katibu Tawala Mkoa Bw. Msovela amesema kuwa, mradi wa DREAMS unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala uwe ni chachu kwa wadau wengine kuusaidia Mkoa kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuwasaidia wasichana ili wabaki shuleni na hatimaye watimize ndoto zao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa