Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewapongeza wananchi wa kata ya Chela katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Wilayani Kahama kwa ushirikiano wao wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya nchini.
Mhe. Telack ametoa pongezi hizo baada ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Mibako Mabubu kueleza kuwa wamekuwa wakikodi nyumba kwa ajili ya watumishi wa afya wa Zahanati ya kijiji cha Mhandu kwa malipo ya sh. 30,000(elfu thelathini) kwa mwezi kabla ya nyumba iliyojengwa na taasisi ya Benjamin Mkapa kukamilika.
Akipokea nyumba hiyo kwa niaba ya nyumba 30 zilizojengwa Mkoa mzima, Mhe. Telack amewaomba wadau wengine kuendelea kushirikiana na Serikali kujenga nyumba za watumishi ambapo amesisitiza ombi hilo kwa kuanza kuchangia ujenzi kwa mabati 50 kutokana na wananchi kunyanyua boma kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nyingine ya Mtumishi wa afya.
Naye Meneja wa benki ya CRDB tawi la Shinyanga, amemuunga mkono Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kuahidi kuchangia mifuko 30 ya saruji ambapo wadau wengine wameahidi kuhakikisha wanachangia ili kukamilisha ujenzi huo.
Wakati huo huo, Mhe. Telack amefungua jengo la upasuaji katika kituo cha afya cha kata ya Chela, kijiji cha Chela lililogharimu kiasi cha shilingi 122 bilioni pamoja na vifaa vya msingi vya upasuaji.
Mhe. Telack amesema ni faraja kubwa kuwa na jengo hilo la upasuaji kwa sababu akinamama wengi na watoto wachanga wamekuwa wakipoteza maisha wakati wa kujifungua.
" Sisi kwetu ni faraja kubwa kwa sababu tunapoteza kina mama na watoto wachanga wakati wa kujifungua. Ni uchungu mkubwa kupoteza siku 1 tu kati ya miezi 9 yote mama aliyobeba ujauzito."
Mhe. Telack pamoja na wadau wengine waliokuwepo katika ufunguzi huo wamechangia jumla ya magodoro 36 na mashuka 76 ili kuhakikisha upasuaji unaanza mara moja katika mazingira mazuri.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa, kuwepo kwa huduma ya upasuaji katika kituo hicho cha afya,itasaidia kutaokoa akina mama 8 kati ya 10 waliokuwa hatarini kupoteza maisha kutokana na kujifungua.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amesema wananchi wataondokana na kero ya muda mrefu kwani huduma hii ya upasuaji imesogea karibu zaidi kwao.
Jengo hilo la upasuaji ni kati ya mawili yaliyojengwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa katika Mkoa wa Shinyanga, moja likiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kata ya Bunambiyu.
Akielezea taarifa ya Taasisi hiyo Mkoani hapa, mwakilishi wa Taasisi hiyo amesema kuwa, kwa kipindi cha miaka 10 imewezesha jumla ya watumishi 27 kupata mafunzo ya afya, wakati watumishi 41 wamefanya kazi katika vituo mbalimbali vya kutolewa huduma za afya. Aidha Taasisi imejenga nyumba 30 za watumishi pamoja na majengo mawili ya upasuaji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Bw. Simon Berege kwa niaba ya Wakurugenzi wa Kishapu na Shinyanga, ameishukuru Taasisi na wadau wote walioshirikiana kwa pamoja kuhakikisha Halmashauri inaboresha huduma za afya.
Bw. Berege amesema kuwa, pamoja na changamoto ya kuwa na watumishi wachache Halmashauri hiyo imeweza kuwa mfano bora kwa Halmashauri nyingi katika kuboresha huduma za afya ikiwemo uandikishaji wa wananchi katika mfuko wa bima ya afya yaani CHF pamoja na uandikishaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa