Jumuiya ya watumia maji ya kijiji cha Mwagala, kata ya Mwagala katika Manispaa ya Shinyanga imetumia kiasi cha sh. Milioni 5.2 kujenga Ofisi kwa ajili shughuli za mradi wa maji kutokana na mapato ya mauzo za maji.
Ofisi hiyo ambayo ipo katika hatua za mwisho za ukamilishaji, imezinduliwa katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji yaliyofanyika Kimkoa kijijini hapo.
Akisoma taarifa ya mradi wa maji wa kijiji hicho, mtunza fedha wa jumuiya ya watumia maji Bi. Uwezo Issa Misanga amesema kuwa, mradi wa maji ambao chanzo chake kikuu ni Ziwa Viktoria una vituo 9 vya kuchotea maji na unahudumia wakazi 3960 na baadhi ya wananchi wameweza kuvuta maji hadi majumbani kwao.
Bi. Misanga amesema kuwa, Kamati ya maji ya kijiji hicho iliyokuwepo awali ilivunjwa na kuundwa kamati ya sasa ambayo imeweza kufanikisha ujenzi huo baada ya kuona kuna haja ya kuwa na ofisi kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za fedha, nyaraka na shughuli nyinginezo za huduma ya maji.
Aidha amewaomba wadau mbalimbali kusaidia kuongeza nguvu ili kukamilisha ujenzi ambao umesimama kutokana na kupungukiwa fedha.
Maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji yamefanyika jana Kimkoa katika kijiji cha Mwagala na kuhudhuriwa na Viongozi, wadau, wananchi na Watalaamu mbalimbali ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Taraba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa