Serikali mkoani Shinyanga imewaonya wananchi wote wakaohusika na uharibifu wa vyanzo vya maji kwa kufanya shughuli za kilimo na kunywesha mifugo kwenye vyanzo vya maji na kusababisha ongezeko la uharibifu wa mazingira.
Mhe. Zainab Telack ameyasema hayo mapema wiki hii, katika kijiji cha Songwa Wilaya ya Kishapu ikiwa ni maadhimisho ya upandaji miti kitaifa yaliyofanyika Wilayani humo.
Ameonya kuwa shughuli hizo zinahatarisha uhai wa vyanzo hivyo vya maji pamoja na uhai wa binadamu kutokana na matumizi ya madawa yanayotumika katika kilimo hicho.
“Kishapu mna mabwawa matatu lakini kwa bahati mbaya wachimbaji almasi na wanaolima kando kando ya mabwawa wameyaharibu, hivyo niwaombe kwa sababu tumetambua kuchimba kwenye mabwawa ni makosa na kulima ni makosa pia ni marufuku kufanya shughuli hizo,” amesisitiza.
“Mnapofanya kilimo cha nyanya au mahindi mnatumia madawa yenye sumu na kuyachafua maji kwa hiyo hayafai kutumika na siku hamna maji mnayatumia wakati huo mmeshaweka sumu, mnaogesha watoto wanapata madhara, acheni kulima kando ya mabwawa haya,” ameongeza Mhe. Telack.
Aidha, Mhe. Telack amesisitiza umuhimu wa kupanda miti kando ya vyanzo vya maji hasa mabwawa na kuwa ndiyo chanzo cha maji kwani husaidia yasikauke hivyo huwezesha mvua kunyesha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe Nyabaganga Taraba amesema hapo nyuma wananchi hawakuwa na mwamko katika shughuli za uhifadhi mazingira hivyo kuchangia kuwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Taraba amesema kuwa baada ya kupanda miti katika maeneo yanayozunguka bwawa hilo hatua hiyo imeweza kusaidia kurudi upya kwake na hivyo wananchi kuendelea kupata faida.
Amesisitiza kuwa suala la upandaji miti pamoja na utunzaji misitu ni la wananchi wote na ndio maana viongozi wote wanashiriki katika zoezi na kuahidi viongozi watandelea kuwa bega kwa bega kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa