Na. Paul Kasembo, SHY RS.
Muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude amesema kuwa jumla ya ya wasichana 198,865 wamelengwa kufikiwa na kupatiwa Chanjo ikiwa ni lengo la asilimia 80 katika kipindi cha tarehe 22 hadi 28 Aprili, 2024 ambayo ni wiki ya chanjo Afrika huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kujitokeza kupeleka watoto wao ili wawezekupatiwa chanjo hii muhimu.
Mhe. Mkude amesema kuwa Kampeni hii ina lengo la kuongeza kinga kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 ambqpo watapatiwa chanjo dozi moja (1) ambapo awali walikuwa wakipatiwa dozi mbili (2) na sababu ya mabadiliko haya ni matokeo ya tafiti za kisayansi zilizothibitisha kuwa dozi moja ya HPV inatosha kutoa kinga kamili dhidi ya maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi.
"Mkoa unatarajia kutoa chanjo kwa wasichana 198,865 Kampeni ambayo tutaianza rasmi tarehe 22 hadi 28 Aprili, 2024 itakayolenga wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 na itafanyika katika Shule za Msingi na Sekondari za Serikali na zisizo za Serikali," amesema Mhe. Mkude.
Utekelezaji wa chanjo hii unatajwa kuwa ni mkakati muafaka katika kutokomeza kabisa maradhi na kupunguza vifo vya watoto, na hivyo kupunguza gharama kubwa ambazo familia za Kitanzania zingetumia katika kutibu maradhi yatokanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo huku akiwaagiza Watendaji ngazi zote wahakikishe wasichana wote walio nje ya shule wanapatiwa chanjo hii.
Nchini Tanzania chanjo hii iliidhinishwa mwaka 2014 na kuanza kutumika rasmi mwaka 2014 katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo baadae mwaka 2018 ilianza kutumika nchi nzima kwa kutoa dozi mbili (2). Chanjo hii imeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa matumizi ya binadamu.
HABARI PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa