Mkoa wa Shinyanga umelenga kutoa chanjo mpya ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana 29,451 kwenye uzinduzi wa chanjo hiyo utakaofanyika hapo Jumatatu ya tarehe 23 Aprili, 2018 katika viwanja vya Zima moto, eneo la Nguzo nane, Manispaa ya Shinyanga.
Wasichana hao ni wote ambao ni wanafunzi na wasio wanafunzi, watapata chanjo hiyo inayojulikana kama HPV (Human Papillomavirus) kwa lengo la kuwakinga na satarani ya mlango wa kizazi ambayo imekuwa tatizo kubwa kwa wanawake hasa katika nchi zinazoendelea.
Mratibu wa Mkoa wa Afya ya Mama na Mtoto Bibi Joyce Kandoro amebainisha kuwa jumla ya wanawake 528,000 wamethibitika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi kila mwaka katika nchi zinazoendelea hususani Tanzania na pia kila mwaka wanawake 7,304 wanapata tatizo hilo nchini.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashid Mfaume amewataka wananchi wote wenye watoto wa umri wa miaka 14 kuwapeleka watoto wao katika vituo vya kutolea huduma hiyo ili kuwakinga na saratani ya mlango wa kizazi.
Naye mmoja wa waratibu wa chanjo hiyo kutoka Wizara ya Afya Bw. Elias Masumbuko amesema kuwa, virusi vya saratani ya mlango wa kizazi huwapata wanawake wakiwa katika umri mdogo lakini madhara yake yanaonekana baadaye wanapokuwa watu wazima, hivyo ni vema kuwakinga mapema ili kuzuia virusi hivyo. Vile vile saratani ya Mlango wa kizazi ni ya kwanza kwa kusababisha vifo kwa wanawake nchini ikifuatiwa na saratani ya matiti.
Ameongeza pia kuwa, kwa wasichana ambao wamevuka umri wa miaka 14 pamoja na wanawake walio katika umri wa kuzaa wanashauriwa kwenda kwenye vituo vya afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu endapo watabainika wana dalili za virusi hivyo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa