Na Johnson James, Shinyanga
Wasimamizi 1632 wa Vituo 391 na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga mjini wameapishwa na kumepewa mafunzo maalum na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ikiwa ni maandalizi ya mwisho kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Octoba 26,2025 katika shule ya Savannah Plains High School iliyopo Manispaa ya Shinyanga pamoja na maeneo mengine ambapo Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Shinyanga mjini Ally Liuye aliwataka wasimamizi hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na uzalendo mkubwa ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani, haki na uwazi.
Amesisitiza kuwa usomaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni jambo la lazima kwa kila msimamizi, kwani ndicho chanzo kikuu cha mamlaka na mwongozo wa uchaguzi nchini.
“Lazima mtambue kuwa macho ya Watanzania na dunia yako kwenu. Zoezi hili linaongozwa na Katiba, hivyo mnapaswa kulielewa kwa undani ili kufanikisha uchaguzi huru, wa haki na unaokubalika,” amesema Liuye.
Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi muhimu ya kuhakikisha siku ya uchaguzi inafanyika kwa utulivu, huku usalama na taratibu zote zikizingatiwa ili wananchi waweze kutumia haki yao ya kikatiba bila bughudha.
Halima Juma ambaye ni Mshiriki wa Mafunzo hayo amesema yatawasaidia kuongeza maarifa ili kuyafikia malengo ya kuwapata viongozi bora kupitia uchaguzi mkuu utakaofanyika Octoba 29 mwaka huu.
Nae Brasio Genda amesema mafunzo hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo wa namna bora ya kusimamia zoezi la upigaji kura na kwamba yamekuja wakati mwafaka.

OFISI YA MKUU WA MKOA, MKOA WA SHINYANGA, 04 MTAA WA BOMA
Anuani: P.O.Box 320, 37180,SHINYANGA, TANZANIA
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa