Mkoa wa Shinyanga unatarajia kutoa chanjo ya Surua na Rubella kwa watoto 286,124 wenye umri wa miezi 9 hadi miaka minne na miezi 11 kwa siku tano za kampeni ya hiyo ya Kitaifa iliyozinduliwa mapema leo tarehe 17/10/2019.
Akizindua chanjo hiyo kimkoa, katika kijiji cha Lyabukande, kata ya Lyabukande, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amewataka wananchi kuwapeleka watoto kupata chanjo ili kuwanusuru na vifo vitokanavyo na magonjwa hayo.
"Rais wetu wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, anayethamini sana afya za wananchi wake hasa katika kuzuia magonjwa yanayoambukizwa, ameendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kwamba kama Nchi tunaboresha afya za wananchi wetu. Hivyo Serikali imeanza kutoa chanjo kwa magonjwa yanayoambukiza ikiwemo Surua na Rubella lengo ni kuhakikisha kuwa tunapunguza ulemavu na vifo vinavyotokana na magonjwa haya ambayo yanaweza kuzuiwa kwa chanjo" amesema Mhe. Telack
Aidha Mhe. Telack amesema kuwa, Mkoa wa Shinyanga utatoa chanjo tatu kwa siku zote tano za kampeni hii ambazo ni Surua, Rubella na Polio ambapo watoto wanaotarajiwa kupata chanjo ya Polio ni 152547.
Telack amewasisitiza wananchi wote kuwa chanjo hizi ni salama kabisa na zinatolewa bure.
Awali akitoa taarifa ya kampeni hiyo, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Afya katika Sekretarieti ya Mkoa Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa, miaka ya nyuma kabla ya chanjo hizi, magonjwa ya Surua na Rubella yalisababisha vifo vingi vya watoto.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa