Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela ameahidi kuwachukulia hatua kali na stahiki watumishi wa afya katika Mkoa wa Shinyanga watakaoabainika kutoa lugha chafu kwa wagonjwa na kwenda kinyume na taratibu na sheria za utumishi wa Umma.
Bw. Msovela ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha uhamasishaji kwa viongozi wa dini kuhusu mfuko wa bima ya afya kwa wananchi wa CHF iliyoboreshwa kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga jana.
Msovela amesema kuwa, watumishi hao hawatavumiliwa kwa sababu watakuwa wanakwenda kinyume na sheria za Utumishi wa Umma na katiba.
“Ni kweli kuna matatizo ambayo Serikali imeyaona kuhusu Wahudumu wa Afya ya kukosa uadilifu, atakayebainika anakwenda kinyume na sheria na taratibu za utumishi wa Umma atachukuliwa hatua stahiki na hakuna huruma itakayotolewa”.
Aidha, ameomba ushirikiano pia kutoka kwa viongozi hao wa dini kwa kusaidia kutoa taarifa kwa Mganga Mkuu wa Mkoa na yeye mwenyewe Katibu Tawala Mkoa ili waweze kufuatilia na kujiridhisha ambapo ametoa namba za simu kwa viongozi hao. “Nia ya Serikali ni kutoa huduma bora kwa wananchi, sheria lazima zisimamiwe”
Awali wakati wa majadiliano ya uhamasishaji wa CHF iliyoboreshwa, baadhi ya viongozi wa dini wameonesha kukerwa na baadhi ya watumishi wa afya wasiojali wagonjwa na kutoa kauli chafu hatimaye kusababisha wananchi kuogopa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa