Na. Paul Kasembo, RS Shinyanga.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu, Ndugu David Lyamongi, aliyemwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni, amewataka wazazi na walezi kuwekeza kwa dhati katika malezi na makuzi ya watoto kuanzia wakiwa tumboni, ili kuimarisha maadili na kuleta tija kwa Taifa katika siku zijazo.
Lyamongi alitoa wito huo Mei 15, 2025 wakati akifungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia kwa Mkoa wa Shinyanga. Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Kalinjuna uliopo katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile.
Viongozi wengine ni kutoka madhehebu ya dini, Kamati ya Amani Mkoa, wawakilishi wa Baraza la Wazee, Baraza la Watoto, Vyama vya Watu Wenyeulemavu, wadau wa maendeleo - Shirika la ICS, na Klabu ya Wandishi wa Habari, wataalamu wa masuala ya kijamii, wanafunzi kutoka vyuo na shule za sekondari pia walishiriki katika kongamano hilo ambalo lililenga kuhamasisha jamii kuishi kwa kuakisi kaulimbiu ya mwaka 2025: “Mtoto na Malezi: Msingi wa Familia Bora, Taifa Imara.”
“Niwatake wazazi na walezi wote mkoani Shinyanga kuhakikisha wanawekeza ipasavyo katika malezi na makuzi ya watoto wetu kuanzia wakiwa tumboni, ili tuweze kujenga Taifa lenye msingi imara wa maadili na maendeleo endelevu,” alisema Lyamongi.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Dkt. Yudas alieleza kuwa maadhimisho hayo yana lengo la kuwaleta pamoja wadau wote wa malezi ya watoto, kwa ajili ya kutafakari na kubadilishana uzoefu juu ya jitihada zinazofanywa katika kuimarisha malezi na makuzi bora kwa watoto.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Lydia Kwesigabo, alibainisha kuwa kila mwaka Mei 15, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia, ikiwa ni fursa ya kutathmini mchango wa jamii katika maendeleo ya watoto na familia kwa ujumla.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa