Na. Shinyanga RS.
Waziri wa Madini Mhe. Dotto Mashaka Biteko amefungua Zahanati iliyojengwa na Kikundi cha Wanawake Wachimbaji Wadogo wa Madini (TAWOMA MSHIKAMANO GROUP) na kukabidhi Gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa wananchi wa Kata ya Lunguya litakalotumika katika Zahanati ya Nyamishiga vyenye thamani ya zaidi ya Tzs. Milioni 280 kwa Halmashauri ya Msalala Mkoani Shinyanga huku akiwaahidi kuwapatia Leseni ya uchimbaji Madini.
Mhe. Biteko ameyasema hayo leo tarehe 3 Julai, 2023 katika hafla hiyo iliyofanyika katika Kijiji cha Nyamishiga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita, viongozi wa Dini, Chama cha Mapinduzi, wachimbaji na wananchi ambapo pamoja na kuwapongeza sana wana kikundi wa Mshikamano lakini pia aliwaeleza namna ambavyo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyowajali wachimbaji wadogo wakiwamo wa Lunguya.
"Mimi niseme tu kuwa, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye aliyeruhusu ninyi mchimbe na sasa niseme tu kuwa katika hili nasema kwa ujari na furaha kubwa kuwa ninyi mnastahili kupewa Leseni, mnastahili kuchimba ili mshiriki uchumi wa madini Mhe. Rais anawapenda sana wana Shinyanga na hata sasa amewaletea viongozi wachapa kazi kweli kweli Mhe. Christina Mndeme anayajuwa madini na haki za wachimbaji anazijuwa pamoja na Mkuu wa Wilaya Mhe. Mboni Mhita ni mpambanaji sana ," alisema Mhe. Biteko.
Aidha TAWOMA MSHIKAMANO walimpongeza sana Mhe. Mndeme kwa namna anavyowajali wachimbaji hao huku wakiomba kujwngewa uzio, kupelekewa umeme na maji ilimkuboresha huduma za kijamii.
Kwa upande wake Mhe. Mndeme alisema kuwa Serikali ya Mkoa wa Shinyanga inawajali sana wachimbaji wadogo wadogo na kwamba suala la ukosefu wa huduma ya maji na umeme amelipokea huku akitumia jukwaa hilo kuwaahidi kupeleka huduma hizo kama walivyoomba.
"Nawaagiza RUWASA NA TANESCO Mkoa wa Shinyanga kuleta huduma ya maji na umeme katika Zahati hii na Eneo hili ili wananchi hawa waendelee kupata huduma hizi muhimu, na kuhusu uzio tutajenga kwa mwaka wa fedha ujao kupitia Halmashauri yetu ya Msalala hivyo wananchi ondoeni hofu kabisa Serikali ipo nanyi," alisema Mhe. Mndeme
Kukamilika kwa Zahanati hii kunakwenda kuwaondolea usumbufu na adha waliuokuwa wakiipata wananchi hawa ambapo walilazimika kutembea umbali wa Kilomita 10 kwenda kufuata huduma ya matibabu katika Kituo cha Afya Lunguya.
Awali wananchi walianza ujenzi wa Zahanati hii mwaka 2018 ikiwa ni sehemu ya kupambana na kukabiliana na usumbufu huo unaotajwa kudumu kwa muda mrefu kwa kutumia nguvu kazi zao wenyewe ambapi jumla ya zaidi ya 21 zilichangishwa kupitia Sungusungu ambazo zilitumika kujenga jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje yaani OPD
Ilipofika Machi, 2022 kikundi cha Mshikamano kilianza rasmi ukamilishaji wa Zahanati hii ambayo inatajwa kwenda kuwahudumia wananchi zaidi ya 4970.
|
|
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa