Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amesema Mkoa wa Shinyanga mwaka huu 2016/ 2017 umetenga shilingi 5,987,366,000 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maji Mkoani hapa.
Mhe. Telack amesema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Josephine Matiro wakati uzinduzi wa wiki ya maji uliyofanyika Kimkoa katika Wilaya ya Shinyanga kwenye kata ya Usanda, kijiji cha Manyada.
Mhe. Telack amesema hadi sasa fedha iliyopatikana na inaendelea kufanyiwa kazi ni sh. 1,756,894,718 sawa na asilimia 29.3 ya bajeti..
Telack amewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuithamini miradi hii na kuitunza ili iwe endelevu kwani inatumia fedha nyingi.
“Viongozi wasimamie utekelezaji wa Sheria ya utunzaji wa mazingira ili kunusuru vyanzo vya maji kwani Serikali inatumia fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maji” Telack amesema katika hotuba yake.
Katika uzinduzi huo wa wiki ya maji Mhe. Josephine Matiro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Zainab Telack, amezindua mradi wa maji ya bomba wa kijiji cha Manyada uliogharimu shilingi 629.8 milioni, ambao utawanufaisha wananchi 3,650 wa vitongoji saba wa kijiji hicho.
Aidha, Mhe. Matiro pamoja na msafara ulioambatana naye, wamepanda miti katika chanzo cha maji cha mradi huo ili kwa lengo kutunza mazingira ya chanzo hicho.
Akizungumzia hali ya maji kwa sasa Mkoani Shinyanga, Mtaalamu wa maji katika Sekretarieti ya Mkoa, Bw. Marwa Kisibo amesema kuwa, kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji mijini ni asilimia 68 na vijijini ni asilimia 52.
Ameongeza kuwa, Serikali ina mpango wa kufikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijijini na asilimia 95 mijini kufikia mwaka 2020 kutokana na program ya maji inayojulikana kama WSDP (Water Sector Development Program) iliyoanza mwezi Julai, mwaka jana 2016.
Amesema kuwa, program hiyo imelenga katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji mijiji na vijijini.
Naye Katibu wa Kamati ya maji ya Kijiji cha Manyada Bw. John Daniel amesema mradi huu utawanufaisha sana wananchi wa kijiji hicho na kuiomba Serikali kuwasaidia kupata umeme kwa ajili ya kuendeshea mtambo wa kusukuma maji badala ya kutumia mafuta ya Dizeli.
Kauli mbiu ya wiki ya maji mwaka huu ni “Maji safi na maji taka, punguza uchafuzi yatumike kwa ufanisi”.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa