Jumla ya sh. Milioni 20.6 kati ya hizo, fedha taslimu zikiwa mil. 10.8 na ahadi sh. Mil. 9.4 na mifuko 465 ya saruji yenye thamani ya sh. Milioni 6.8 zimechangwa katika harambee maalumu iliyofanyika wakati wa mahafali ya kidato cha nne na maadhimisho ya miaka 50 ya shule ya Sekondari ya Shinyanga iliyopo katika Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Harambee hiyo imefanyika jana tarehe 13/10/2017 na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack kwa lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa nyumba mbili za kuishi walimu kila moja yenye uwezo wa kubeba familia 5, ujenzi wa jengo la maabara ya Zahanati na vyumba vitatu vya kupumzisha wagonjwa pamoja na jengo la wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Kabla ya kuendesha harambee hiyo, Mhe. Telack amesema kuwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni sawa na watoto wengine kiakili hivyo wanahitaji miundombinu itakayowawezesha kutekeleza vema majukumu yao wakiwa shuleni.
Aidha, amewataka wahitimu kutumia mitandao ya kijamii kutafuta fursa za maendeleo na masomo ya juu badala ya kutumia kwa mambo yasiyo ya faida kwao.
Mgeni rasmi wa shughuli hiyo Dkt. Charles Kimei aliyewakilishwa na Bw. Phillip Magani kutoka benki ya CRDB makao makuu katika hotuba yake amesema ni fahari na furaha kwa nchi yetu kwa shule ya Shinyanga Sekondari kufikisha miaka 50 kwani imeweza kusomesha maelfu ya Watanzania ambao wengi wao ni viongozi na watendaji wakubwa katika Sekta mbalimbali nchini na hata nje ya nchi.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Nyabaganga Taraba amewataka wanafunzi wa miaka ya nyuma wa shule hiyo akiwemo Dkt. Kimei kutosahau walipotoka na kuwasisitizwa kuwa shule ya “ShyBush” inawahitaji kusaidia katika juhudi za maendeleo kwani ni shule ya Watanzania wote.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa