SHINYANGA MC.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) ameisisitiza Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kuendelea kutoa elimu ya uelewa wa sheria kwa wananchi baada ya kumalizika kwa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria jambo litakalopunguza malalamiko kwa Mhimili huo.
DC Mtatiro ameyasema haya Februari 3, 2025 wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ambapo pamoja na yote amewapongeza Mahakimu na Majaji kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuwafikia wananchi na kuwapatia huduma za kisheria.
“Tunawapongeza kwa kazi nzuri ambayo mmeifanya kwa wiki nzima ili kuwafikia wananchi na kuwapatia huduma za kisheria, lakini nawasisitiza kwamba utoaji wa elimu ya uelewa na huduma za sheria iwe endelevu ili watu wengi zaidi iwafikie na kupunguza malalmiko ya wananchi,” amesema DC Mtatiro.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Mhe. Frank Mahimbali amesema kuwa wameanza rasmi mwaka wa 2025 wakiwa hawana kesi zozote za nyuma kutokana na juhudi na kazi nyingi walizofanya kuhakikisha wanamaliza kesi kwa muda mufaka
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Shinyanga Shaban Mvungi amesema kwa mwaka 2024 TLS imewafikia wananchi takribani 7,307 kupitia Wiki ya Sheria na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ikiwa na lengo la kushiriki katika utoaji wa Msaada wa Kisheria.
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga yalianza tarehe 25 Januari, 2025 na yamehitimishwa leo tarehe 3 Februari, 2025 ambapo yaliambatana na utoaji waelimu na msaada wa kisheria kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa