Na. Paul Kasembo, KISHAPU.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa, heshima ya zao la pamba mkoani Shinyanga sasa inakwenda kurejea kama ilivyokuwa hapo zamani huku akiwasisitiza Maafisa Ugani Kilimo kuwa wabunifu zaidi, kutumia taaluma zao kuleta mapinduzi ya kweli na kwamba watapimwa utendaji kazi wao kupitia ongezeko la uzalishaji wa zao hili ambalo linatajwa kuwa zao muhimu la kibiashara ambapo kwa Shinyanga linazalishwa zaidi wilayani Kishapu.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 10 Novemba, 2024 katika semina elekezi kwa Maafisa Ugani Kilimo na Watendaji wa Kata wote iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama akiwemo Mkuu wa Wilaya Mhe. Josph Mkude na Balozi wa Pamba nchini Ndugu Aggrey Mwanri na watalaam kutoka Bodi ya Pamba Kanda ya Ziwa.
"Nitumie nafasi kuwaeleza kuwa, heshima ya zao la pamba mkoani Shinyanga sasa inakwenda kurejea kama ilivyokuwa hapo zamani, lakini pia nanyi Maafisa Ugani Kilimo na Watendaji Kata mbadilike, muwe na uwezo wa kujiongeza, kuwa wabunifu na mtumie elimu yenu kuleta mabadiliko ya kweli na katika hili tutawapima kupitia uzalishaji wa zao hili," amesema RC Macha.
Kando na hili pia ametoa siku mbili (2) tarehe 10 - 11 Novemba, 2024 kwa wakulima wote wa zao la pamba kuhakikisha kuwa wanachoma wanang'oa na maoteo na masalia yote kabla ya kuanza msimu wa kilimo kwa mwaka huu wa 2024/2025 kqzi ambayo kwa mujibu wa sheria ya pamba na kanuni zake ilipaswa kutekelezwa kabla ya Septemba, 15..
Kwa upande wake Balozi wa Pamba ndg. Mwanri amesema kuwa, maotea na masalia katika zao pamba ni jambo ambalo halikubaliki kabisa kuachiwa liendelee, na ikitokea hivyo mkulima atazalisha pamba ambayo ni mapepe, isiyokuwa na ubora na ambayo ahikubaliki sokoni na hapo ndiyo malalamiko ya wakulima huanzia.
Ufuatiliaji, usimamizi na utekelezaji wa urejeshaji heshima ya zao la pamba mkoani Shinyanga ni sehemu ya mikakati ya RC Macha ya kuhakikisha kuwa zao hili muhimu la biashara mkoani Shinyanga maarufu kama (dhahabu nyeupe) linarejea kama zamani.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa