Mkandarasi anayetengeneza barabara kwa kiwango cha lami katika Manispaa ya Shinyanga chini ya mpango wa uimarishaji Miji (ULGSP) Jassie & Co. Ltd (JASCO), ametakiwa kukamilisha kazi iliyobaki kiasi cha kilomita 8.9 kwa wakati uliopangwa vinginevyo atachukuliwa hatua.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo amemuagiza Mkandarasi huyo mapema leo alipotembelea Mkoani Shinyanga kwa lengo la kukagua ujenzi wa barabara hizo ulioanza tangu mwaka 2016.
Mhe. Jafo amesema atarudi baada ya miezi mitatu baada ya Mkandarasi kumuhakikishia kuwa, baada ya muda huo atakuwa amekamilisha kazi hizo ikiwemo uwekaji wa taa za barabarani baada ya changamoto zilizokuwepo kufanyiwa kazi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemueleza Waziri Jafo kuwa, endapo Mkandarasi huyo atakwenda kinyume atachukuliwa hatua za kisheria kwani amekuwa na kazi maeneo mengi hali inayochangia kufanya kazi isiyoridhisha.
Mradi huo wa ujenzi wa barabara za lami chini ya ULGSP ulianza mwaka 2016 ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga iliingia mkataba na JASCO kujenga jumla ya kilomita 13.1 kwa gharama ya zaidi ya sh. Bil. 15, lakini hadi mwishoni mwa mwaka jana 2017 ni km 4 tu ndiyo zilikuwa zimewekwa lami wakati km 4.43 zimejengwa tuta kwa ajili ya maandalizi ya kuwekwa lami.
Aidha, ujenzi huo ulisimama kwa takribani miezi 9 tangu Septemba mwaka 2017 kutokana na Mkandarasi kudai kutatuliwa baadhi ya changamoto ikiwemo marekebisho ya mkataba ambapo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa, ziliweka sawa maeneo yaliyohitaji kutekelezwa na ujenzi umeanza tena mwezi Mei,2018 ukitarajiwa kukamilika tarehe 23 Oktoba, 2018.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bw. Gofrey Mwangulumbi amemueleza Mhe. Jafo kuwa, changamoto ya fedha ilitokana na kuja kwa fedha ambazo hazikuwa na mchanganuo hivyo kuchelewesha ufungaji wa mkataba.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa