Serikali Mkoani Shinyanga kwa kushirikiana na viongozi wa dini wameazimia kutokomeza mauaji yaliyoshamiri Mkoani hapa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wivu wa kimapenzi na imani za kishirikina kwa kuunda Kamati maalumu ya Amani kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi.
Uamuzi huo umefikiwa mapema jana katika kikao cha pamoja cha viongozi hao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack kwenye ukumbi wa Mikutano wa Ofisi yake.
Kamati hiyo yenye wajumbe kumi, inayohusisha viongozi wa dini wa pande zote imepewa jukumu la kutoa elimu kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga ili kuisaidia jamii kuacha kuamini ushirikina, kuacha kujichukulia sheria mkononi pamoja na kuwajengea imani ya kumcha Mungu.
Awali akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa Mhe. Telack amesema hivi sasa uhalifu hususani mauaji yameshamiri Mkoani hapa hivyo Serikali imeona kuna haja ya kushirikisha na viongozi wa Dini ili wasaidie pia kusema na wananchi kwani ndiyo waamini wao kwenye nyumba za Ibada.
Mhe. Telack amesema anaamini Kamati hiyo itafanya vizuri katika kutoa elimu kwa wananchi na pia Serikali itatoa ushirikiano katika kila hatua.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa, SSP Lutusyo K. Mwakyusa akitoa taarifa ya uhalifu ya Mkoa kuanzia mwezi Januari - Aprili, 2018 amesema kuwa, tathmini inaonesha, makosa ya kero kwa jamii kama wizi yamepungua japokuwa mauaji kutokana na imani za kishirikina na wivu wa mapenzi zimeongezeka. Aidha, ametaja sababu nyingine za mauaji ni pamoja na ongezeko la migogoro ya ardhi, visasi kutokana na uhasama, wananchi kujichukulia sheria mkononi, uhaba au umbali wa upatikanaji wa huduma za afya.
Lutusyo amesema mauaji ya imani za kishirikina yameongezeka kwa asilimia 14 na kutokana wivu wa mapenzi yameongezeka kwa asilimia 11.4 na pia karibu asilimia 90 ya mauaji yanatokana na imani za kishirikina.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa