Na. Paul Kasembo, RS SHY.
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) amemuagiza Meneja wa Tarura Wilaya ya Shinyanga Eng. Samson Pamphir kuanza matengenezo ya barabara ya kuelekea Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza) yenye urefu wa zaidi ya Km 4, kwa kutumia fungu la dharura ili iweze kuwaondolea adha wakazi wa maeneo hayo ikiwemo wagonjwa wanaopelekwa kwa ajili ya huduma za afya kutoka Hospitali ya Rufaa.
Maagizo haya yametolewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Soko Kuu Manispaa ya Shinyanga ambapo Mhe. Mtatiro alikuwa akipokea, kusikiliza na kutatua kero za wananchi moja kwa moja ambapo pamoja na hayo pia aliwataka wale wote wenye kero nzito na ngumu zaidi kuwa na subira wakati Kamati aliyoiunda Mhe. Mtatiro itawafikia kwa haraka na kutatua kero zao zote kabla hajaanza kwenda yeye mwenyewe eneo la tukio.
"Nakuagiza Meneja wa Tarura Wilaya ya Shinyanga uanze haraka matengenezo ya barabara kuelekea Mwawaza hata kama ni kwa fungu la dharura, haiwezekani kila ninaposimama naelezwa suala la barabara hii, sasa nasema matengenezo yaanze haraka ili kuwaondolea adha wakazi wa maeneo hayo," amesema Mhe. Mtatiro.
Kadhalika Mhe. Mtatiro alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwl. Alexius Kagunze kwa utendaji kazi wake mzuri anaoendelea nao katika kuwahudumia wananchi, huku akimtaka kuendelea na kasi hiyo.
Kupokea, kusikiliza na kutatua kero za wananchi kupitia mikutano ya hadhara ni utaratibu mzuri anaoutumia Mhe. Julius Mtatiro tangu aliporipoti katika Wilaya ya Shinyanga, na unatajwa kuwaondolea kabisa kero na changamoto wanazokutana nazo wananchi.
MATUKIO KATIKA PICHA
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa