Na. Paul Kasembo, SHY RS.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) ameshauri kuwepo na mpango wa muda mrefu katika utoaji wa elimu ya mlipa kodi huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kuanzisha utaratibu wa kuanza kufundishwa katika shule zetu na kuirasimisha lengo ni kuwajengea uelewa kuhusu elimu ya mlipa kodi huku njia hii ikitajwa kuleta mapinduzi ya uzalendo na uelewa kwa jamii na hasa walipa kodi wa Taifa letu.
Mhe. Mtatiro ameyasema haya leo tarehe 17 Januari, 2025 wakati akifungua mkutano wa Tume ya Rais ya Kukusanya Maoni ya Maboresho ya Kodi ambayo kwa Mkoa wa Shinyanga uliongozwa na CPA. Leonard Mususa ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi Balozi. Ombeni Sefue ambapo pamoja na mambo mengine amewaongoza wadau katika zoezi la ukusanyaji maoni hayo, mkutano huu umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Davil Lyamongi aliyemwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni.
"Pamoja na pongezi kwa kazi nzuri, naomba nitoe ushauri wangu, kuanzishwe utaratibu wa kufundisha somo la kodi katika shule zetu na lirasimishwe kwenye mitaala yetu ili watakapohitimu watakuwa wamejengeka katika uzalendo na uelewa mkubwa juu ya ulipaji kodi jambo ambalo litapelekea ongezeko kubwa la pato, na hili liwe ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa utoaji elimu wa muda mrefu," amesema Wakili Mhe. Mtatiro.
Akitoa salamu za Tume, CPA. Leonard alisema kuwa dhumuni la kuundwa kwa Tume ni kufanya tathmini ya mifumo ya kodi, mapato na tozo nyingine ili kuiwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki za kuondoa kero/malalamiko, kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi.
Mdau wa masuala ya kodi, unaombwa kutoa maoni yako kuhusu changamoto zilizopo kwenye masuala ya kodi, upendekeze njia za kutatua changamoto hizo. Pamoja na mambo mengine, Tume imewaomba wadau kuendelea kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha kwa kutuma ujumbe mfupi (sms) na Whatsapp kwa namba 0748 755677, 0738 588813, 0682 288784.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa