Na. Paul Kasembo, SHY MC.
KATIBU Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni amejitambulisha mbele ya Baraza la Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga huku akiwaomba ushirikiano wao katika kuhakikisha anatekeleza vema wajibu na majukumu yake ya kila siku hapa Mkoa wa Shinyanga.
CP. Hamduni ameyasema haya leo tarehe 31 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa mkutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo pia ametumia nafasi hii kuwakumbusha Waheshimiwa Madiwani kwenda kuwa sehemu ya utoaji hamasa na elimu juu ya ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba watumie fursa zote za vikao na mikutano yao kutoe ujumbe huu ili wakati utakapofika wananchi waweze kujitokeza na kushiriki kikamilifu zaidi.
"Waheshimiwa Madiwani Manispaa ya Shinyanga pamoja na watumishi wenzangu, baada ya kujitambulisha rasmi kwenu sasa niwaombe ushirikiano wenu ili nami niweze kutekeleza vema wajibu na majukumu yangu na pia twende tukasaidie kutoa elimu na hamasa kwa wanachama na wananchi wetu ili waweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tarehe 27 Novemba, 2024," amesema CP. Hamduni.
Kando na hili, pia amewataka Waheshimiwa Madiwani kwenda kushirikiana na Kamati za Usalama katika maeneo yao ukizingatia tunaelekea kwenye Uchaguzi hivyo wananchi wawe na amani na utulivu zaidi kusiwepo na hali yoyote itayopelekea viashiria vya uvunjifu wa amani wakati wote.
Kwa upande wake Naibu Meya Manispaa ya Shinyanga Mhe. Zamda Shabani kwa niaba ya Mstahiki Meya Mhe. Elias Masumbuko na Waheshimiwa Madiwani amemkaribisha kwa mikono miwili CP. Hamduni na kwamba amemhakikishia ushirikiano wa haki na mali wakati wote kutoka kwao na wananchi wa Manispaa kwa ujumla.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa