Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bw. Geofrey Mwangulumbi kumsimamisha kazi Afisa manunuzi wa Manispaa hiyo Bw. Mwita Peter Nyang’anyi ili kupisha uchunguzi kutokana na kutosimamia utaratibu wa kununua mbao kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Kambarage hivyo kuisababishia Serikali hasara ya shilingi milioni 3.
Mhe. Telack ameitaka pia taasisi ya kupambana na kuzuia Rushwa, TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, kuwafanyia uchunguzi ndani ya siku 3, Mhandisi wa ujenzi Bw. Deogratius Mworo na Afisa manunuzi huyo ili kubaini sababu ya iliyofanya kurudisha mbao zilizonunuliwa kwa madai kuwa mbao hizo siyo imara na kisha kuagiza mbao nyingine hivyo kuongezeka kiasi hicho cha fedha kinyume na bajeti iliyokuwa imepangwa.
Telack ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki baada ya kufanya ziara katika kituo hicho kwa lengo la kukagua na kuona hatua ya ujenzi na upanuzi wa kituo baada ya kikao cha pamoja na kamati za ujenzi, manunuzi na mapokezi katika ujenzi huo.
Akizungumza na viongozi na watendaji wa Manispaa hiyo Mhe. Telack amewataka kupokea vifaa hasa mbao na mabati vikiwa na vipimo kutoka shirika la viwango “TBS” na pia kamati za mapokezi zisipokee vifaa visivyokuwa na ubora.
Amesema fedha inayotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa vituo ni ya moto hivyo watendaji wasifikiri wataweza kuitumia kwa maslahi yao binafsi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa