Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amemkabidhi gari jipya STN 2943 Mhandisi Julieth Payovela ambaye ni Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga katika hafla fupi iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga huku akisisitiza kuwa ikatumike kwa kadiri ya lengo kusudiwa la serikali.
Hafla hii imefanyika leo tarehe 28 Oktoba, 2024 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude, pamoja na watumishi mbalimbali kutoka RUWASA na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha watumishi kutekeleza kazi zao kwa ufanisi zaidi na kuwahudumia wananchi kwa wakati na kuwafikia kwa haraka zaidi.
"Kwanza tumshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha watumishi katika Wizara, Sekta na Ofisi zake zote ili kurahisisha utekelezaji na usimamizi wa shughuli za kila siku kama ambavyo imefanyika kwa wenzetu hawa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, niwaombe kwenda kutumia gari hili kwa kadiri ya lengo lililokusudiwa na Serikali na wala isiwe vinginevyo," amesema RC Macha.
Kando na hayo, ameitaka RUWASA Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha kuwa gari hili linatunzwa kwa maslahi mapana ya Serikali ili lidumu muda mrefu na lifanyiwe matengenezo stahiki pale inapohitajika kufanya hivyo huku akiwataarifu waalikwa wa hafla hii kuwa anatambua, anathamini na kuheshimu zaidi kazi, ubunifu, weledi na utendaji kazi wa Meneja RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth.
Kwa upande wake Mha. Julieth amemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha ofisi yake kupata kitendea kazi ambacho kinakwenda kuongeza ufanisi na uboreshaji wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku, huku akimpongeza RC Macha kwa kuendelea kuisaidia RUWASA katika utekelezaji wa kazi zake mkoani Shinyanga.
Upokeaji wa gari hili jipya STN 2943 kwa RUWASA Shinyanga unakwenda kurahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa miradi wa miradi yake.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa