Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita ameongoza juhudi za Serikali kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 kati ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC – Mwanva) na wananchi waliokuwa wakiishi ndani ya eneo la hekari 40 zilizotengwa kwa matumizi ya makazi.
Akiwa katika kata ya Malunga, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mhe. Mhita alizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi, ili kufafanua msimamo wa Serikali kuhusu mgogoro huo ambao awali ulisababisha wananchi kushindwa kuendeleza maeneo yao.
Waziri Ndejembi alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan haina nia ya kuwaonea wananchi, na hivyo wale wote waliokuwa ndani ya hekari 40 lakini walisahaulika katika maamuzi ya mwaka 2021 wakati wa uongozi wa Hayati Dkt. John Magufuli, watatambuliwa rasmi na kumilikishwa maeneo yao kihalali.
“Tutawatuma wataalamu kutoka Wizarani wakiongozwa na Kamishna wa Ardhi kwa ajili ya kuwatambua walengwa halali, siyo wale waliovamia baada ya maamuzi ya awali kufanyika. Serikali ipo kwa ajili ya wananchi na haitaki kuona mtu anateseka kwa migogoro inayoweza kutatuliwa,” alieleza Mhe. Ndejembi.
Kwa upande wake, Mhe. Mhita alisema mgogoro huo ameushughulikia kwa muda mrefu tangu akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, na sasa juhudi hizo zimezaa matunda baada ya Serikali kutoa mwelekeo sahihi wa kuwatambua ambao walisahaulika kimakosa
Wananchi waliokumbwa na mgogoro huo walitoa shukrani kwa Serikali na kumpongeza Mhe. Mhita kwa kufuatilia suala hilo kwa ukaribu, hali iliyowarejeshea matumaini baada ya miaka mingi ya sintofahamu kuhusu hatma ya maeneo yao.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa