Na. Paul Kasembo, Shy RS.
Mwenyekiti wa Bodi ya Akiba na Mikopo Wilaya ya Shinyanga (SDC SACCOS) ndg. Epafras Mazina amesema kuwa wamejipanga kikamilifu kuwanufaisha wanachama wake huku akisisitiza kuwa uwepo wa chama hiki umepunguza kadhia kwa kuepuka kuumizwa na mikopo yenye riba kubwa kwani kinawasaidia kukopa na kuboresha maisha yao kwa kuwa kila mwisho wa mwaka kunakuwa na gawio kubwa kwa wanachama wote.
Ameyasema haya tarehe 7 Desemba, 2024 wakati wa mkutano mkuu wa 22 wa mwaka ambao umelenga kufanya tathmini ya maendeleo ya chama pamoja na kuweka mikakati ya utendaji na utekelezaji kwa kipindi kinachofuata , mkutano ambao umefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
“Chama hiki kimeendelea kuwasaidia watumishi kwani wanaweza kukopa na kuboresha maisha yao kwa namna moja ama nyingine kwa kuwa kila mwisho wa mwaka kunakuwa na gawio kwa wanachama wote na hii imepunguza kadhia kwa wanachama kwa kiasi kikubwa kwa kuwa hawataumizwa tena na mikopo yenye riba kubwa (kausha damu) kutoka kwenye Mashirika au vikundi vya utoaji mikopo na sasa tutawanufaisha zaidi,” amesema Mazina.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ndg. David Rwazo amewapongeza wanachama kwa ushirikiano mzuri wanaoonyesha lakini pamoja na yote amewataka wanachama kuwa waaminifu kwa kujitahidi kurudisha fedha wanazokopeshwa kwa wakati ili kufanya chama kizidi kusonga mbele na kufanikiwa zaidi.
Ikumbukwe kuwa Chama cha SDC SACCOS kilisajiliwa tarehe 20 Juni, 2006 ili kuunganisha rasilimali fedha za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa kutoa huduma za akiba na mikopo yenye riba na masharti nafuu zaidi ambapo mpaka sasa kina jumla ya wanachama ambao ni watumishi 2002 kati ya watumishi 2437 katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa