Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amezitaka taasisi za fedha zinazokopesha kuwaambia ukweli wananchi kuhusu riba na kiasi cha fedha wanachotakiwa kulipa.
Mhe. Telack ametoa agizo hilo katika kikao cha pamoja na wafanyabiashara wa Mkoa wa Shinyanga kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi yake.
Telack amesema hatakubaliana na biashara hizo kwani wananchi wengi wamekuwa wakiumizwa na madeni kutoka kwenye taasisi hizo na kufikia kuuzwa kwa mali zao ili kufidia madeni. “Taasisi hizi haziwasaidii wananchi wengi na matokeo yake kuwaumiza”
“Mikopo iwe ni kwa ustawi wa wananchi na kwa maendeleo yao” amesisitiza Mhe. Telack.
Mhe. Telack amesema kuwa taasisi hizo wanatumia uelewa mdogo wa wananchi kuwaumiza kwa mikopo yenye riba kubwa kuliko uwezo wao.
Aidha, taasisi hizo pia zimeshauriwa kutumia lugha ya Kiswahili ambayo wananchi wengi wanaimudu ili waweze kuelewa wakati wa kujaza fomu za mikopo.
Katika kikao hicho, Wafanyabiashara wametakiwa kuwa na ushirikiano baina yao pamoja na Serikali ili kuweza kutambua fursa mbalimbali zilizopo katika Mkoa na kuwekeza kwa manufaa yao na Mkoa wa ujumla. Telack amesema Ofisi yake iko wazi kutoa msaada wa aina yoyote kwa wafanyabiashara.
Aidha, Mhe. Telack ametoa rai kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Shinyanga kujitangaza kwa kushiriki maonesho mbalimbali ikiwemo maadhimisho ya Wakulima yaani Nane nane yanayofanyika Mwezi ujao, pamoja na kuandaa maonesho ya bidhaa zao kimkoa.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa