Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga kufanya kazi kwa kushirikiana na Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri husika kabla hawajapeleka huduma katika maeneo ya makazi ya wananchi ili kuepukana na migogoro ya ardhi ambayo inaweza kujitokeza.
RC Macha ameyasema haya leo tarehe 9 Januari, 2025 wakati akitoa salamu za mwaka mpya kwenye Kikao Kazi na Watumishi wa Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Julius Mtatiro (Wakili) na Mhe. Joesph Mkude Mkuu wa Wilaya ya Kishapu na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kahama, na Wakuu wa Taasisi za Umma zikiwemo TANESCO, TARURA, TANROAD, SHUWASA, RUWASA, KUWASA, KASHWASA, BODI YA PAMBA na NFRA Mkoani wa Shinyanga pamoja na wakuu wa Sehemu na Vitengo.
“Ninawaagiza SHUWASA na TANESCO mkafanye kazi kwa ushirikiano mkubwa pamoja na Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri husika kabla hamjaanza kupeleka huduma katika maeneo ya makazi ya wananchi ili maeneo hayo myafahamu vizuri na hivyo mtaepuka na kuzuia migogoro ya ardhi isiyokuwa ya lazima ambayo imekuwa ikijitokeza kwa kutofanya kazi kwa pamoja,” amesema RC Macha.
Awali akimkaribisha RC Macha kuzungumza na wajumbe wa kikao ambacho , Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni amesema kuwa wametekeleza kikamilifu maelekezo yaliyotolewa kwa kuandaa kikao kazi hiki ambacho kimelenga kuangazia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo Elimu, Kilimo, Afya, Utatuzi wa migogoro, Tathmini ya Mbio za Mwenge 2024 na maandalizi ya Mbio za Mwenge zijazo kwa mwaka 2025 nk.
Kwa nyakati tofauti, Mkurugenzi wa SHUWASA Mha. Yusuph Katopola na Kaimu Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mha. Antony Tarimo wamekiri kupokea maelekezo, ushauri na mapendekezo ya RC Macha na kwamba kuanzia sasa watafanya kwa karibu na Ofisi za Wakurugenzi kabla ya kuanza mchakato wa kuwafikishia huduma wananchi.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa