#shinyanga_rs
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, kwa niaba ya wananchi wa Shinyanga, amempongeza na kumshukuru kwa dhati Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya nchini, ikiwa ni pamoja na kuleta timu ya Madaktari Bingwa 43 walioanza kutoa huduma katika Mkoa wa Shinyanga kuanzia tarehe 23 hadi 28 Juni 2025.
Akizungumza katika hafla ya kuwapokea Madaktari hao iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Macha aliwataka wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi katika Halmashauri zote sita za Mkoa ili kunufaika na huduma za Kibingwa zitakazotolewa kwa siku hizo sita mfululizo.
“Ninamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika afya za wananchi wetu. Kupitia jitihada zake, tumepokea Madaktari Bingwa 43 kutoka Wizara ya Afya watakaotoa huduma katika Halmashauri zote sita za Mkoa wetu. Naomba Wanashinyanga tujitokeze kwa wingi kutumia fursa hii muhimu,” alisema Mhe. Macha.
Aidha, Mhe. Macha alieleza mafanikio ya Sekta ya afya ndani ya miaka minne ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa kiasi cha takribani Shilingi Bilioni 77 kimetolewa kwa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya afya, ununuzi wa vifaa tiba na dawa.
“Kwa mwaka 2021 tulikuwa na Hospitali za wilaya mbili pekee, lakini ndani ya miaka minne ya uongozi wa Mhe. Rais, sasa tuna Hospitali saba za Halmashauri na pia huduma zimeanza kutolewa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa yenye vifaa tiba vya kisasa pamoja na Madaktari Bingwa,” alisisitiza RC. Macha.
Kwa upande wake, Dkt. Grace Mariki ambaye ni kiongozi wa timu ya Madaktari Bingwa kutoka Wizara ya Afya, alisema kuwa timu hiyo inajumuisha Madaktari wa fani mbalimbali zikiwemo magonjwa ya wanawake, watoto, upasuaji, magonjwa ya ndani, kinywa na meno, ganzi, masikio, pua pamoja na koo.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa