WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watoa huduma za afya wa nchi wananchama wa kanda ya Afrika Mashariki kuondoa vikwazo vinavyozuia wagonjwa wanaotafuta matibabu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.
"Hatua hii ni kwa manufaa ya wananchi wetu na kwa uchumi wa kikanda na ukuaji wa utalii tiba."
Ametoa wito huo leo (Ijumaa Agosti 30, 2024 ) alipokuwa mgeni rasmi katika Mkutano wa 12 wa Shirikisho la Watoa Huduma za Afya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Njerere (JNICC). Dar es Salaam
Amesema nchi wananchama ikiwemo Tanzania zimejitahidi kuwekeza katika sekta ya afya na kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya Kanda kwa matibabu.
"Kwa sasa ni wagonjwa wachache sana wanaosafiri nje ya nchi zetu kwa ajili ya matibabu, kwani karibu magonjwa yote makubwa sasa yanaweza kutibiwa ndani ya Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wa Sekta ya Afya kuwekeza nchini Tanzania.
Amesema Serikali imetengeneza sera rafiki za uwekezaji hususan katika Sekta ya Afya kutokana na uhitaji wa huduma hizo nchini.
"Tunawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya afya, Sera nzuri tunazo, Sheria na kanuni nzuri tunazo, mahitaji ya uwekezaji kwenye sekta ya afya ni makubwa na tunataka tupate teknolojia mpya na huduma za kibingwa."
Kadhalika amewataka wadau wa afya wa kanda kujadili mbinu mbalimbali za kuimarisha mifumo ya afya na kuwa na mikakati ya pamoja ya kukabiliana na magonjwa.
"Tumieni jukwaa hili kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na magonjwa ya mlipuko, magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ambukiza pamoja na magonjwa mapya yanayotokana na mabadiliko ya hali ya tabia nchi".
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema uwekezaji uliofanywa na serikali kuanzia ngazi ya chini umewezesha ugunduaji wa magonjwa yakiwa katika hatua za awali.
"Rufaa kwenda nje ya Nchi zimepungua kwa kiasi kikubwa kipindi cha nyuma watu waliokuwa wanafika Ocean road walikuwa kwenye hatua za mwisho za ugonjwa, lakini kutokana na uwekezaji sasa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanakuja wakiwa na magonjwa katika hatua za awali"
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI 30, 2024.
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa