Na. Shinyanga RS.
Umoja wa Shirikisho la Machinga Mkoa wa Shinyanga wametoa TAMKO kuunga mkono Serikali juu kuingia mkataba baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai katika ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha utendaji kazi wa Bandari Tanzania huku wakisisitiza kuwa wanaunga mkono juhudi zote zinazofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuifanya Nchi kuwa yenye maendeleo zaidi kupitia uwekezaji ambao DUBAI PORT WORLD (DP World) wamekubaliana na Serikali ya Tanzania.
Akisoma TAMKO hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa, Mwenyekiti wa Shirikisho Mkoa wa Shinyanga Ndg. Boniphace Petro alisema kuwa wao Umoja wa Machinga Mkoa wa Shinyanga wanaridhishwa sana na namna ambavyo Serikali inashughulikia mambo yao wao machinga, uchumi wa nchi, namna ambavyo Serikali inatoa fedha za maendeleo na ndiyo maana katika hili la DP World wanaunga mkono na kwamba leo wameamua kutoa TAMKO RASMI huku wakilaani vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya watu wasioitakia heri nchi yetu kwa kuamua kwa makusudi kupotosha ukweli kuhusu DP World na Bandari Tanzania.
“Sisi Umoja wa Shirikisho la Machinga Mkoa wa Shinyanga katika kikao chetu na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga leo tarehe 19 Juni, 2023 tumesikiliza na kupokea maelezo ya Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu Mkataba wa baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendeshaji na uboreshaji kazi wa Bandari Tanzania, tumeelewa vema sana na sasa tumeamua kutoa TAMKO RASMI la kuunga mkono jambo hili na kuanzia sasa tutakwenda kuwa mabalozi wazuri wa kuelezea wenzetu katika maeneo tunayotoka juu ya nia njema ya Serikali yetu,” alisema Boniphace.
Awali akitoa salamu za Serikali Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme alisema kuwa, pamoja na mambo mengi ambayo Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan lakini pia Mkoa umepokea zaidi ya fedha za kitanzania Bilioni 612 ambazo zimepelekwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya afya, elimu, miundombinu, uwezeshaji wananchi kiuchumi, maji na umeme katika Mkoa wa Shinyanga.
Aidha Mhe. Mndeme alisema kwamba, Serikali inawatambua, inawathamini sana Machinga na ndiyo maana yeye mwenyewe hayupo tayari kabisa kuona machinga yoyote anadhurumiwa, kunyanyaswa wala kusumbuliwa na yoyote kwakuwa Serikali inataka wafanye biashara zao kwa amani na utulivu kwa fuata kanuni, taratibu na sheria za nchi.
“Kuweni na amani, fanyeni kazi zenu bila hofu yoyote kabisa Serikali ipo, inawajali na hakuna yeyote atakayekuja kuwasumbua, kuwafungia biashara zenu wala kuwanyanyasa katika maeneo yenu kikubwa tu mzingatie sheria, kanuni na taratibu za nchi katika utekelezaji wa shughuli zenu za kila siku,’’ alisema Mhe. Mndeme.
Huu ni utaratubu aliojiwekea Mhe. Mndeme wa kukutana na kuzungumza na makundi mbalimbali Mkoani hapa kwa lengo la kuwasikiliza, kupokea changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi kwa ushirikiano ambapo tarehe 20 Juni, 2023 atakutana na kundi la wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara Mkoa wa Shinyanga.
Picha ikionesha sehemu ya wajumbe wa Machinga wakiwa ukumbini wakati wa kikao na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme (hayupo pichani).
Boma Street, Mwanza Road
Anuani: P.O.Box 320, Shinyanga
Simu: +255 28 2762222
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ras@shinyanga.go.tz
Hakimiliki@2018. Mkoa wa Shinyanga. Haki zote zimehifadhiwa